ALBINO 400 WAMEUAWA KIKATILI
Mkurugenzi wa Shirika la (JTF) Josephat Torener akitoa Neno kwa waumini wa Kanisa la KKKT Mjini Shinyanga na kuwataka waliombee Amani Taifa ambayo imeshaanza kuonekana kuteteleka kutokana na kukithiri kwa Mauji ya watu wasio na hatia.
SOMA HABARI KWA KINA
MKurugenzi wa
Shirika la (JTF) linaloshughulika na makundi maalumu hapa nchini Josephati
Torner amebainisha jumla ya watu zaidi 400 wenye ulemavu wa ngozi (Albino),
katika nchi za Afrika 25 wamesha uawa kikatili kutokana na Imani Potofu za Kishirikina.
Torner aliyazungumza
hayo mjini Shinyanga kwenye Kanisa la Kiinjiri la Kirutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi
Masharika ya Ziwa Victoria, kwenye Ibada ya Misa ya Pili kanisani hapo, kuwa tangu
mauji hayo yaliposhamiri mwaka (2008-16) zaidi ya Albino 400 wameuawa kwa
kukatwa katwa Mapanga.
Aidha kufuatia
Mauji hayo Torner ambaye pia ni Mlemavu wa ngozi (Albino) aliwataka viongozi wa
Madhehebu mbalimbali hapa nchini washirikiane na Serikali kikamilifu kutokomeza
Mauji ya watu hao wasio na hatia, kwakusambaza neno la bwana kwa watu wote ili
waache kuuwana kama wanyama.
“Serikali peke
yake haiwezi kumaliza tatizo la Mauji ya watu wenye Albino maana kuna mtandao
mkubwa wakiwamo wazazi na ndugu ambao wanaishi na walemavu hao kutengeneza
njama za kutekeleza Mauji kwa Imani Potofu ili wapate utajiri, lakini endapo
elimu ya kiroho ikitolewa vizuri mauaji haya yatakoma,”alisema Torner
Hata hivyo Torner
aliwataka watanzania kujituma kufanya kazi kwa bidii njia ambayo itawasaidia
kuyafikia Malengo yao, na siyo kutamani kuwa na Maisha Mazuri kwakutegemea Imani
za Kishirikina, Kitendo ambacho kimekuwa kikisababisha mauaji ya watu wasio na
hatia.
Naye Mchungaji
wa Kanisa hilo Michael Lyimo akitoa neno la Bwana kwenye ibada hiyo, alisema
uhai wa mtu unatwaliwa na Mwenyezi Mungu pekee kwa mapenzi yake, ikiwa maandiko
yanasema kila binadamu lazima ataonja umauti, na hivyo kukemea watu ambao
wamegeuka wanyama na kuchinjana ovyo.
Pia mchungaji
Lyimo aliwataka waumini wa Kanisa hilo na wananchi kwa ujumla kutenda mema yale
yanayompendeza mwenyezi mungu na kuacha mambo Maovu ambayo yamekuwa yakivuruga
amani ya nchi na kulitia doa taifa.
Na Marco Maduhu ambaye pia ni Mwandishi wa Theguardian / Nipashe - Shinyanga