Wasimamishwa kazi baada ya mama mjamzito kujifungua kwenye korido



Aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri ya Shinyanga vijijini Kiomoni Kibamba ameacha simanzi kwa wauguzi wawili wa kituo cha afya cha Lyabukande wa halmashauri hiyo, baada ya kuwasimamisha kazi kutokana na uzembe walioufanya wa kukimbia kituo na kusababisha wajawazito kujifungua kwenye makorido.



Tukio la wajawazito hao kujifungulia kwenye Makorido lilitokea julai 2 mwaka huu ambapo mmoja wa wajawazito hao Magdalena Leonard kwa bahati mbaya mtoto wake alifariki kutokana na kukosa huduma stahiki za matibabu baada ya kukosa msaada kutoka kwa wauguzi ambao hawakuwepo kituoni ndani ya masaa nane.

Akizungumza na media Kibamba alisema, baada ya kupata taarifa hizo za watumishi kutokuwepo kwenye kituo cha afya, waliunda tume kwenda kuchunguza na kubaini kuwa tuhuma hizo niza kweli nakusababisha kifo cha mtoto mchanga baada ya wazazi wakijifungulia kwenye makorido.

Kibamba ambaye kwa sasa amehamishiwa kituo cha kazi Jijini Mwanza, alisema baada ya kujiridhisha na uchunguzi huo ameamua kuwasimamisha kazi wauguzi wawili wa kituo hicho ambao ni Zulfa Musa na Peter Mazengo wa kitengo cha maabara ambao walikuwa zamu kwa kutokuwepo kituoni na kusababisha kifo.

“Nilikwisha tamka siku nyingi awamu hii ya tano ni ya kazi tu na mfanyakazi atakaye shindwa kuendana na kasi ya Rais Magufuli atupishe wabaki wachapakazi tu, lakini baadhi ya watendaji wamekuwa wagumu kuielewa slogan ya Rais na kuchukulia mzahamzaha hawa ndio watakuwa kafara kwa watumishi wengine,”alisema Kibamba na kuongeza kuwa

“Hata kama mimi naondoka shinyanga nitamwachia Mkurugenzi mwingine atakaye kuja alisimamie suala hili la kuendelea kuwachukulia hatua kali za kinidhamu maana hatutaki kufanya kazi na watumishi wazembe wa kuichafua serikali kwa wananchi wake.”

Aidha Kibamba alisema hivi sasa wauguzi hao wameshafunguliwa Jalada la mashitaka ya kimaadili ya utumishi na kupewa siku 14 kujieleza kwa utaratbu wa ajira ya utumishi na baada ya hapo watasubiri baraza la madiwani ndio wenye maamuzi ya mwisho ya kuwafukuza ama kutoa adhabu kali dhidi yao.


Na Marco Maduhu -Msukuma Blog
Powered by Blogger.