BASI LA JM LUXRY LACHINJA WANNE SHINYANGA
Basi la JM Luxury Couch likiwa limepinduka
Mabaki ya lori lililokuwa na watu wanne ambao wote wamepoteza maisha
Watu wanne wamefariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya JM Luxury Couch lenye namba za usajili T.159 OYZ kugonga lori lenye namba za usajili T.218 ABY aina ya TATA katika barabara ya Shinyanga kwenda Mwanza katika eneo la njia panda ya kwenda wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo ajali hiyo imetokea leo asubuhi wakati basi linalofanya safari zake Mwanza -Dar es salaam kugonga lori lililokuwa linakata kona kwenda wilayani Kishapu.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari,Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa basi lenye namba T.159 OYZ aina ya Yutong mali ya kampuni ya JM Luxury Couch likiendeshwa na Sarehe Kassim(46) mkazi wa Dar es salaam.
“Hili basi lilikuwa katika mwendo kasi,likagonga lori lenye namba T.218 ABY aina ya TATA mali ya kampuni ya Birichand Oil Mill ya Mwanza likiendeshwa na dereva ambaye sasa ni marehemu na hajatambulika jina wala makazi yake”,alieleza Kamanda Muliro.
“Chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa basi likitaka kulipita lori ambalo lilikuwa likikata kona kuelekea wilaya ya Kishapu na kuligonga upande wa kulia na kusababisha vifo vya watu wanne ,wote wanaume waliokuwa ndani ya lori akiwemo dereva wa lori na wote hajatambulika miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga”,aliongeza Kamanda Muliro.
Kamanda Muliro aliongeza kuwa katika ajali hiyo watu wanne waliokuwa katika basi walijeruhiwa akiwemo dereva wa basi.
Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Sarehe Kassimu(46),dereva wa basi mkazi wa Dar es salaam,Mohamed Ahmed Shahel (39),kondakta wa basi,mkazi wa Kimara jijini Dar es salaam,Valencia Magingi (34) mkazi wa Mwanza ,wamelazwa katika hospitali ya Kolandoto na Joseph Mkunda (58) mkazi wa Dar es salaam ambaye amelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
Alisema hali za majeruhi siyo mbaya sana na wanaendelea na matibabu.