Wazee wa CHADEMA Wamtuhumu Msajili wa Vyama Kwa Kuandaa Mitego Haramu ya Kukifuta Chama Hicho

Baraza la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) limetoa pongezi kwa Kamati Kuu ya chama hicho kuahirisha maandamano na mikutano ya nchi nzima iliyopewa jina la Ukuta.


Maandamano hayo ambayo yalipangwa kufanyika kuanzia Septemba Mosi, mwaka huu yaliahirishwa na Kamati Kuu ya chama hicho kwa madai ya kuombwa na viongozi wakuu wa madhehebu ya dini.


Akizungumza katika Makao Makuu ya chama hicho jana, Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Roderick Lutembeka alisema, hatua ya kamati hiyo kuahirisha maandamano hayo ni muhimu na inaonesha jinsi chama hicho kina viongozi wavumilivu.


“Kwa kutambua moyo wa kiuongozi waliouonesha na dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania wote, tunapenda kuwapongeza viongozi wetu wakuu kwa uamuzi huu wa busara ambao umeuthibitishia umma kuwa chama kina viongozi imara,” alisema Lutembeka


Katika hatua nyingine, baraza hilo limesema limebaini kuwepo kwa njama zinazopikwa dhidi ya chama hicho kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Baraza la Vyama vya Siasa nchini, kukifuta chama hicho.


“Taarifa zinaonesha njama hizo zinalenga kukihujumu Chadema kwa kuandaa mitego haramu ya kisiasa ili hatimaye yatolewe mapendekezo ya kukifuta katika orodha ya vyama vya siasa,” alisema Lutembeka na kuongeza;


“Tarehe 15 Agosti mwaka huu Jaji Mtungi alitangaza kuwa, Baraza la Vyama vya Siasa lilikuwa limeitisha kikao ambacho kingefanyika tarehe 29-30 Agosti kujadili masuala ya hali ya kisiasa nchini. Siku mbili kabla ya kikao Mwenyekiti wa baraza akatangaza kukiahirisha hadi tarehe 3-4 mwezi huu.


“Jambo la kushangaza baada ya busara kutumika kupitia viongozi wa dini kushawishi Chadema kuahirisha kwa kutoa mwanya wa mazungumzo hadi tarehe 1 mwezi ujao, Kamati ya Uongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa ikaibuka tena na kutangaza kuahirisha kikao cha baraza hadi itakapotangazwa tena.


“Wakati taarifa zote hizo zikitolewa na viongozi wa baraza, ofisini hapa (Chadema) hakuna hata barua moja kutoka kwa msajili ya kutuita katika kikao chochote kati ya hivyo. Kuanzia kile cha tarehe 29-30 Agosti, tarehe 3-4 Septemba wala hiyo ya kuahirisha.


“Katika mazingira haya nani ambaye hatashawishika kuamini ofisi ya msajili inatii maagizo ya watawala,”


Powered by Blogger.