Ahukumiwa kifungo cha maisha kumlawiti mtoto wa miaka mitatu
Mahakama ya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa imemhukumu kifungo cha maisha jela, Frank Mlyuka (24) baada ya kupatikana na hatia ya kubaka na kulawiti mtoto wa kike wa miaka mitatu.
Mbali na hukumu hiyo, Mlyuka ametakiwa kulipa Sh5milioni kama fidia kwa wazazi wa mtoto huyo.
Akisoma hukumu hiyo juzi Februari 14, 2018 Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Hussein Marengu amesema Mahakama imetoa hukumu hiyo baada ya kujiridhisha kuwa Mlyuka alitenda makosa hayo na mwenyewe kukiri mbele ya Mahakama.
Mwendesha mashtaka wa Serikali, Nashoni Simon amesema mshtakiwa alitenda makosa hayo Februari 9, 2018 katika Kijiji cha Kihesa Mgagao wilayani Kilolo.
Kwa mujibu wa mwendesha mashataka huyo, siku hiyo mshtakiwa alipita nyumbani kwa mama mkubwa wa mtoto huyo, na kumkuta mtoto huyo akicheza na wenzake.
Amesema mshtakiwa alimwita mtoto huyo ndani na kumwingiza jikoni ambapo alimbaka na kumlawiti, kumsababishia maumivu makali na kwamba baada ya tukio hilo aliondoka.
Amesema mtoto huyo baada ya kufanyiwa kitendo hicho alitoa taarifa kwa mama yake mkubwa, ambapo msako ulianza na mshtakiwa huyo kukamatwa huku mtoto huyo akipelekwa zahanati ya Pomerini, baadaye kuhamishiwa
Hospitali ya Rufaa Iringa alikolazwa kwa siku moja.
Hakimu Marengu ameeleza kuwa miongoni mwa vielelezo vinavyothibitisha kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo ya kubaka na kulawiti ni hati ya maelezo ya mshtakiwa mbele ya walinzi wa amani na taarifa ya daktari.
Alipotakiwa kujitetea, Myuka anayeishi na wazazi wake amesema ametenda kosa hilo akiwa amelewa na hana cha kujitetea.
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah amekiri kuongezeka matukio ya ubakaji wilayani humo na kubainisha kuwa wastani wa watoto wanne hubakwa kila mwezi.
Chanzo: Mwananchi