ASKOFU TAG SHINYANGA AKANUSHA TUHUMA ZA KUVURUGA MAKANISA

Askofu wa Kanisa la Tanzania Asseblies of God (TAG) Jimbo la Shinyanga Kaskazini Mungo Makundi, amekanusha tuhuma za ubinafsi wa kuhodhi madaraka ambao umesababisha baadhi ya wachungaji kwenye Kanisa hilo, kuondoka na waumini na kufungua makanisa yao mengine.
Amebainisha hayo leo marchi 27 wakati akizungumza na Nipashe ofisini kwake, kuhusiana na tuhuma ambazo zimeelekezwa dhidi yake na baadhi ya waumini wa kanisa hilo wakiwamo viongozi na wachungaji, kuwa Askofu huyo amekuwa akiliongoza kanisa vibaya na kusababisha kuwapo na mpasuko.
Askofu Makundi amesema tuhuma ambazo zimelekezwa dhidi yake siyo za kweli, ikiwa yeye anafuata kanuni sheria na katiba ya kanisa hilo, na kubainisha kuwa wachungaji waliohama kwenye kanisa hilo pamoja na waumini wao, waliondoka wao wenyewe kwa matakwa yao.
“Makanisa yetu yapo huru mtu anaruhusiwa kuondoka kwa matakwa yake mwenyewe hakatazwi, na kati ya wachungaji hao walioondoka baadhi yao wametubu na kuomba kurudi nasi tumewapokea sababu wamejua wamekosea wapi,”Amesema Makundi.
Ameongeza baadhi ya wachungaji na viongozi hao baada ya kukosa madaraka sababu ya kuvunjwa kwa jimbo la Shinyanga na kugawanywa na Kahama, ndipo wakawa na makundi na kuanzisha migogoro ndani ya kanisa na kutaka kutuchafua, ndipo Askofu mkuu Dk Barnabas Mtokambali akatoa baraka kwao ya kujiondoa.
Awali baadhi ya waumini ama washirika wa kanisa hilo ambao waliomba kutotajwa majina yao walimtupia lawama Askofu wao wa jimbo la Shinyanga Kaskazini (TAG) Mungo Makundi, kuwa ameshindwa kuongoza makanisa hayo kutokana na ubinafsi wa kuhodhi madaraka, na kupelekea kutoelewana na wachungaji wake.
Naye mmoja wa wachungaji wa kanisa hilo Yohana Mboje, ambaye pia ni msimamizi wa makanisa hayo ya (TAG), amekiri kuwapo na mgogoro ndani ya kanisa hilo, na kubainisha mpaka sasa makanisa Matatu yameshavurugika ambayo ni (TAG) Ndembezi, Mipa pamoja na Nyanhende Kitangili.

Askofu wa Kanisa la Tanzania Asseblies of God (TAG) Jimbo la Shinyanga Kaskazini Mungo Makundi akionyesha nyaraka mbalimbali ambazo amekuwa akishirikiana na viongozi wenzake na kukana kuwa na ubinafsi, mkono wa kushoto ni Katibu wake mpya Gabliel Gidimayo.

JIWE LA MSINGI LA KANISA HILO LA (TAG) SHINYANGA .
Na Marco Maduhu ambaye pia ni Mwandishi wa gazeti la Nipashe Shinyanga