CHANZO DIWANI KUDAIWA KUTEMBEZA KICHAPO KWA NES


Wakati wanawake wakisherekea siku ya wanawake duniani,Nesi aliyejulikana kwa jina moja la Hilda akiendelea kuhudumia wagonjwa katika kituo cha afya cha Bunambiyu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga amejikuta katika wakati mgumu baada ya kushambuliwa kwa kuchapwa vibao na diwani wa kata ya Bunambiyu Richard Sangi Sangi (CCM).



Inaelezwa kuwa chanzo cha tukio hilo lililotokea leo Alhamis Machi 8,2018 majira ya saa tatu na nusu asubuhi, ni diwani huyo kumtuhumu nesi huyo kuwa hahudumii wagonjwa vizuri na kumtaka aondoke kituoni na alipogoma ndipo diwani alipoamua kumshambulia nesi huyo mbele ya wagonjwa.




Inasemekana  kuwa diwani huyo alipigiwa simu na wananchi wakimwelezea kuwa mgonjwa wao aliyelazwa katika kituo hicho cha afya kwa zaidi ya wiki moja hapatiwi huduma vizuri na ndipo diwani huyo alipoomba kuongea kwa simu na nesi aliyepo zamu,nesi akamsihi diwani afike ofisini/kituoni na alipofika akaanza kumshambulia nesi huyo.


“Huyu diwani amekuwa kama rais,wananchi wanapeleka malalamiko yote kwake,alipigiwa simu kuwa mgonjwa wao hapatiwi huduma vizuri hali inayosababisha aendelee kulazwa”,kilieleza chanzo cha habari cha Malunde1 blog.


Hata hivyo habari zaidi zinasema,wakati nesi Hilda akiendelea kuhudumia wagonjwa,ghafla nesi mwingine ambaye hakuwa zamu aliingia katika wodi ya wagonjwa na kuwaambia ndugu wa mgonjwa huyo kuwa ndugu yao ana upungufu wa damu hivyo anatakiwa kupewa rufaa kwenda hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.


“Kutokana na hali hiyo ndipo ndugu wa mgonjwa wakaamua kumpigia simu diwani na kutaka kuongea kwa simu na nesi wa zamu,nesi akaomba diwani afike ofisini,alipofika ndipo akaanza kuonesha ubabe kwa kumshambulia nesi ambaye alikuwa zamu na alikuwa anasimamia kituo cha afya kutokana na mganga mkuu wa kituo kutokuwepo kazini”,kilieleza chanzo chetu.


Taarifa ambazo mtandao huu umezipata ni kwamba tayari nesi huyo ameelekea kituo cha polisi kutokana na tukio hilo la kushambuliwa na kudhalilishwa na diwani huyo.

Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kishapu,Josephine Matiro amesema tayari amepokea taarifa za tukio hilo na anazifanyia kazi
Powered by Blogger.