RC MNYETI AVUNA WANACHAMA 3,500 KUTOKA CHADEMA


Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye mkoa huo, akimkabidhi aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Narakauwo, Saruni Ole Sanjiro kadi ya CCM kati ya wananchi 3,500 wa Chadema waliojiunga na CCM jana.


Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akizungumza na wananchi wa kijiji cha Narakauwo Wilayani Simanjiro juu ya mgogoro wa uongozi na kumuagiza mkuu wa Wilaya hiyo mhandisi Zephania Chaula aitishe kikao cha wanakijiji hao ili kujadili tatizo lao.


WANACHAMA 3,500 wa Chadema katika Kijiji cha Narakauwo, Kata ya Loiborsiret Wilayani Simanjiro, wamejiunga na CCM kwa lengo la kumuunga mkono Rais John Magufuli na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti.

Wananchi hao ambao awali walikuwa CCM, waliondoka kwenye chama hicho na kujiunga na Chadema, baada ya kigogo mmoja kukata majina ya baadhi ya wagombea waliokuwa wanawaunga mkono kwenye Kijiji hicho na kata hiyo mwaka 2015.

Akizungumza jana wakati akiwapokea wanachama hao wapya kwenye mkutano uliofanyika kijiji cha Narakauwo, Mnyeti ambaye pia ni Mjumbe wa kamati ya siasa ya CCM Mkoani Manyara, alitoa onyo kwa wanasiasa wanaowayumbisha wananchi wa eneo hilo.

Mnyeti alisema kuna baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo bado wamelala kwani wanadhani huu ni wakati wa kufanya siasa ili hali ilishakwisha mwaka 2015 na huu ni wakati wa kufanya kazi.


"Kuna baadhi ya viongozi walikaa vikao usiku ili kukwamisha suala hili, nawapa onyo la mwisho, kama kuna mtu anataka ubunge asubiri mwaka 2020 siyo leo," alisema Mnyeti.


Hata hivyo, Mnyeti alimuagiza mkuu wa wilaya hiyo mhandisi Zephania Chaula kuhakikisha anamaliza mgogoro wa uongozi wa kijiji hicho.


"Mkuu wa wilaya baada ya siku nne rudi hapa ufanye mkutano wa kijiji kama hawa wajumbe wa serikali ya kijiji ndiyo tatizo fuateni taratibu zote waondoke uchaguzi ufanyike upya," alisema Mnyeti.

Alimuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Yefred Myenzi kuhakikisha uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi za uenyekiti unaofanyia Machi 25, ujumuishe na kijiji hicho.

Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Ally Kidunda alisema eneo hilo halina upinzani ila wanachama hao waliondoka kwa sababu ya hasira.

Kidunda aliahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa wanachama hao wapya ili kutimiza dhana ya CCM mpya na Tanzania mpya.

Mmoja kati ya wanachama hao wapya, Mathayo Lesenga alisema awali waliondoka CCM baada ya wagombea waliokuwa wanawaunga mkono kukatwa majina yao.

Lesenga alisema wananchi wa eneo hilo walikuwa na imani na CCM lakini baada ya kuona kunafanyika ukiritimba walijitoa na kuhamia Chadema ila sasa hivi wamerudi ili kumuunga mkono Rais Magufuli na Mnyeti.
Powered by Blogger.