DC KISHAPU AONYA WAFANYABIASHARA KULANGUA MAZAO YA WAKULIMA MASHAMBANI

Mkuu wa wilaya ya Kishapu Nyabaganga Taraba, ametoa tahadhari kwa wafanyabiashara ambao wameanza tabia ya kutembelea wakulima mashambani kwa ajili ya kulangua mazao yao kwa bei ya kuwanyonya, na kubainisha atakae kamatwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Amesema kumekuwa na tetesi kwa baadhi ya wafanyabiashara kuanza kuwatembelea wakulima mashambani na kuingia nao ubia wa kulangau mazao yao kwa kuwapatia fedha kidogo, jambo ambalo Serikali imeshalipiga marufuku, ambapo wakulima wote wanatakiwa kuuza mazao yao kwenye vyama vya msingi vya ushirika.
Taraba alitoa tahadhari hiyo jana wakati akiongea na Nipashe ofisini kwake juu ya Serikali ilivyojipanga kumsaidia mkulima kunufaika na mazao yake pale atakapo anza kuyauza, iliwaweze kupata faida na kuinuka kiuchumi, kuwa mkakati uliopo ni wakulima wote watauza mazao yao kwenye vyama vya ushirika na siyo kwa wafanyabiashara .
“Nimeanza kusikia tetesi kuwa hivi sasa kuna wafanyabiashara wameanza kuzunguka na magari yao mashambani kwenda kwa wakulima kulangua mazao yao, na suala hilo naaza kulifanyika kazi nanitakaye mkamata nitamshughulikia, tunataka wakulima wapate kunufaika na kilimo chao kuinuka kiuchumi,”alisema.
Aliongeza kuwa wafanyabiashara hao wengi wao hua ni wanyonyaji, kwa kumpatia pesa kidogo mkulima na kisha wao kupata faida nyingi na kumuacha mkulima huyo kuendelea kuwa maskini siku zote, na kufanya kilimo chake kutokuwa na tija kwake na kunufaisha matajiri.
Aidha alisema mpango wa Serikali ni kuhakikisha kila mkulima anauza mazao yake kwenye vyama vya msingi vya ushirika, ambapo mpaka sasa kwenye wilaya hiyo viumeshaundwa vyama 78 ambavyo ndivyo vitakuwa vikilangua mazao hayo ya wakulima, pamoja na kulipa pesa zao kupitia account za benk ili kuondoa matumizi yasiyo ya lazima.
Pia alitoa wito kwa wakulima wilayani humo pindi watakapouza mazao yao na kupata fedha nyingi, wazitumie kwa maendeleo ikiwamo kuondoa nyumba za tembe na kujenga za mabati, kusomesha watoto, kuongeza hekali za mashamba, kufungua biashara ndogondogo, na siyo kuzifanyia anasa pamoja na kuongeza wanawake.
Na Marco Maduhu ambaye pia ni Mwandishi wa gazeti la Nipashe