WANAFUNZI WALIOTAKA MWIGILU, NDALICHAKO WAJIUZULU YAWARUDI

WANAFUNZI sita wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wamepewa barua za onyo kwa kuhamasisha maandamano kinyume cha sheria.
Wanadaiwa kuhamasisha maandamano ya kutaka Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba ajiuzulu kutokana na kifo cha mwanafunzi wa
Chuo cha Usafirishaji (NIT), marehemu Akwilina Akwilini, aliyeuawa kwa
risasi Februari 16, mwaka huu.
Barua hizo zilizosainiwa na Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma), Profesa
David Mfinanga, kwenda kwa wanafunzi hao, ambao wamekataa majina yao
yasitajwe, zimesema onyo hilo ni la mwisho.
Kwamba endapo wataendelea kujihusisha na vitendo hivyo,
watasimamishwa masomo mara moja kulingana na kipengele 14(xi) wakati
mashtaka dhidi yao yakiandaliwa na kushughulikiwa.
“Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, umepata taarifa kuwa wewe
ni miongoni mwa wanafunzi wanaojihusisha na vitendo kinyume cha sheria
ndogo ndogo za wanafunzi wa Chuo Kikuu ya mwaka 2011, hususan makosa
yaliyoainishwa kwenye vipengele 4.2(vxiii), 4.2(xix) na 4.2 (xxvi).
“Vitendo hivyo visivyokubalika ni pamoja na kupanga na kuhamasisha
maandamano kinyume cha sheria, kujihusisha na vitendo vinavyokishushia
hadhi chuo kwa kuanzisha kikundi/vikundi visivyoruhusiwa dhidi ya
wanafunzi wenzako, Serikali na viongozi wa nchi.
“Kwa barua hii, unatakiwa kuacha mara moja vitendo hivi na endapo
utakaidi, utakuwa umejiongezea makosa mengine kama yalivyoainishwa
kwenye sheria ndogo ndogo za wanafunzi wa chuo vipengele vilivyotajwa,”
ilieleza sehemu ya barua hizo.
Barua hizo zimetumwa nakala kwa Makamu Mkuu wa Chuo, Naibu Makamu
Mkuu wa Chuo (Taaluma), Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Utafiti), Mwanasheria
Mkuu wa Chuo na Kaimu wa Baraza na Mkurugenzi wa Shahada za Awali kwa
kumbukumbu.
Mmoja wa wanafunzi waliopewa barua hizo, alisema wamezichukua polisi
Kituo cha Chuo Kikuu, baada ya kupigiwa simu Machi 14, mwaka huu
wakitakiwa kuzichukua, lakini hawakuweza kwa sababu walikuwa wamefunga
chuo.