DIWANI WA KATA YA SONGWA ABDULI NGOLOMOLE ANUSURIKA KIFO AJALI YA NOAH




Diwani wa Kata ya Songwa halmashauri ya Kishapu Mkoani Shinyanga Abdul Ngolomole (28) na wenzake watatu wamenusurika kifo, mara baada ya gari waliyokuwa wanasafiri aina ya Noah yenye namba za usajili T 219 CHT ikiwa katika mwendo kasi iliacha njia na kupinduka.
Tukio la ajali hiyo limetokea April 3 mwaka huu, wakati diwani huyo akiwa na wenzake Watatu wakitoka Maganzo kwenye wilayani Kishapu, walipofika eneo la Mwagungulwa barabara ya Kolandoto kwenda wilayani humo, walipata ajali hiyo ya gari na kuvunjika baadhi ya viungo vyao vya mwili na hakuna aliyefariki dunia.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simoni Haule, alisema diwani huyo Abdul Ngolomole amevunjika bega la mkono wa kushoto, Abdala Omary amevujika paja la mguu wa kulia, na Tayaya Rashidi ambaye amepata majeraha sehemu za mbavu na kiuno.

Alisema katika ajali hiyo hakuna aliyepoteza maisha, na majeruhi wote wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga wakiendelea kupatiwa matibabu, ambapo dereva wa gari hilo aliyefahamika kwa jina moja la Phabian, alikimbia mara baada ya kusababisha ajali hiyo na jeshi linaendelea kumtafuta.

Katika tukio jingine watu wawili wamefariki dunia katika ajali ya Pikipiki iliyotokea katika eneo la Zogomela wilayani Kahama, wakati wakiwa wamebebwa mshikaki na kufariki dunia papo hapo.

Aliwataja watu waliofariki kwenye ajali hiyo kuwa ni Mwanaisha Maganga, na Zawadi Stanley, ambapo dereva wa pikipiki hiyo yenye namba za usajili T 185 CJF Sanlg, ambaye hakufahamika jina alikimbia kusikojulikana mara baada ya ajali hiyo kutokea.

Aidha kufuatia matukio hayo yote mawili Kamanda Haule anatoa wito kwa madereva wa vyombo vya Moto, kutii sheria bila shuruti za usalama barabarani na kuepusha ajali zisizo la lazima.

Na Marco Maduhu ambaye pia ni Mwandishi wa gazeti la Nipashe Shinyanga





Powered by Blogger.