MKUU WILAYA YA SHINYANGA AMEFUNGUA MKUTANO WA CHANJO YA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI
Mkuu
wa wilaya ya Shinyanga Mheshimiwa Josephine Matiro amefungua mkutano wa
wadau wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi mkoani Shinyanga
uliolenga kujadili namna ya kufanikisha zoezi la chanjo hiyo kwa
wasichana wenye umri wa miaka 14 mkoani humo.
Mkutano huo umefanyika leo Jumanne
Aprili 17,2018 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa
Shinyanga na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa chanjo ya saratani ya
mlango wa kizazi mkoani Shinyanga.
Akifungua mkutano huo,Mkuu wa wilaya ya
Shinyanga Josephine Matiro kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga
alisema Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto kwa
kushirikiana na wadau wa chanjo imeanzisha chanjo mpya ya kuwakinga na
ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi kwa wasichana wenye umri wa
miaka 14.
Matiro alisema saratani ya mlango wa
kizazi ni ya kwanza nchini Tanzania kwa kusababisha vifo ikifuatiwa na
saratani ya matiti ambazo zote zinasababisha zaidi ya asilimia 50 ya
vifo vyote vya akina mama vitokanavyo na saratani hivyo kunahitajika
juhudi na ushirikiano zaidi kupunguza vifo hivyo.
“Lengo la kuanzisha chanjo hii ni
kukinga mabinti kutokana na madhara makubwa yanayoweza kuwapata ambayo
husababisha vifo vingi kwa wanawake,na walengwa wa chanjo hii mwaka huu
ni wasichana wote wanaotimiza miaka 14 ambapo katika mkoa wa Shinyanga
wasichana wasiopungua 29,479 watachanjwa”,aliongeza.
Alisema chanjo hiyo itatolewa bila
malipo katika vituo vya kutolea huduma vya serikali na binafsi ,baadhi
ya shule na maeneo katika jamii ambazo zitatolewa kwa njia ya huduma za
mkoba.
“Saratani hii inachangiwa na vitu
vingi ikwemo kuanza kujamiiana katika umri mdogo,kuwa na wapenzi
wengi,ndoa za mitaala,kuzaa watoto wengi na uvutaji wa sigara”,alieleza.
Alizitaja dalili za saratani ya mlango
wa kizazi kuwa ni kutokwa damu ya hedhi bila mpangilio,kutokwa damu
baada ya kujamiiana,maumivu ya mgongo,miguu na kiuno,kuchoka,kupungua
uzito,kukosa hamu ya kula,kutokwa uchafu wa rangi ya kahawia au wenye
damu kwenye uke na maumivu ya miguu au kuvimba.
Hata hivyo alisema dalili mbaya zaidi
zinazoweza kujitokeza kuwa ni pamoja na kuishiwa damu,figo kushindwa
kufanya kazi,kupatwa na fistula na uvimbe wa tezi.
Kwa upande Mganga mkuu wa mkoa wa
Shinyanga,Dkt. Rashid Mfaume alisema kati ya wasichana 7304 wanaougua
saratani ya mlango wa kizazi nchini kila mwaka,4216 sawa na asilimia 58
wanafariki dunia hivyo ni muhimu zaidi kupata kinga kuliko tiba.
Alisema uzinduzi rasmi wa chanjo hiyo
mkoani Shinyanga utazinduliwa siku ya Jumatatu Aprili 23,2018 katika
manispaa ya Shinyanga.
Naye Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga
Albert Msovela alisema tayari pesa kwa ajili ya chanjo hiyo zimeshatumwa
kwenye halmashauri kinachotakiwa ni utekelezaji tu ili kuhakikisha mkoa
unafanya vizuri katika zoezi hilo la utoaji chanjo kwa wasichana.
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA MKUTANO HUO HAPA CHINI
Matiro alisema serikali imeamua kuanza kutoa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa sababu saratani ya mlango wa kizazi ndiyo inayoongoza kwa kuua wanawake wengi ukilinganisha na saratani nyingine nchini.
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA MKUTANO HUO HAPA CHINI
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akifungua mkutano wa wadau wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi mkoani Shinyanga -
Matiro alisema serikali imeamua kuanza kutoa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa sababu saratani ya mlango wa kizazi ndiyo inayoongoza kwa kuua wanawake wengi ukilinganisha na saratani nyingine nchini.
Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Dkt. Rashid Mfaume akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi mkoani Shinyanga.
Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Albert Msovela akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi mkoani Shinyanga.
Mkutano ukiendelea...
Wadau wakiwa ukumbini..Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba
Kushoto ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Ngassa Mboje akiwa na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bakari Kasinyo
Wadau wakiwa ukumbini
Mkutano unaendelea
Mtakwimu (Mpango wa taifa wa chanjo), David Kayabu akitoa mada kuhusu zoezi la chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi
Daktari wa Meno mkoa wa Shinyanga, Dkt. Nuru Mpuya ambaye ni Mkufukunzi wa mafunzo ya chanjo ya HPV akitoa mada ukumbini kuhusu chanjo hiyo
Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga,Albert Msovela akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Ngassa Mboje akichangia hoja wakati wa mkutano huo
Mratibu wa afya ya uzazi na mtoto halmashauri ya Mji Kahama Carolyne Marcel akichangia hoja wakati wa mkutano huo
Mratibu wa afya halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Mary Maka akichangia hoja ukumbini
Kaimu Mganga mkuu manispaa ya Shinyanga, Dkt. Daniel Nsaningu akichangia hoja ukumbini