MTOTO WA MIEZI MIWILI ANUSURIKA KIFO BAADA YA KUDAIWA KUNYWESHWA SUMU NA BABA YAKE MZAZI KUFICHA SIRI KUZAA NJE YA NDOA




Maria Shija mkazi wa Kitongoji cha Unyanymbe Kata ya Kizumbi ambaye ni Mama wa mtoto ( jina limehifadhiwa) akiwa amembeba mtoto wake ambaye amedai alitaka kuuawa kwa kunywesha Sumu ya Panya na Baba yake mzazi (Mume aliyezaa naye) kwa madai ya kutaka kuficha Siri kwa Mkewake kuwa amezaa nje ya Ndoa.


SOMA HABARI KAMILI

Mtoto wa miezi miwili jina limehifadhiwa mkazi wa Kitongoji cha Unyanyembe Kata ya Kizumbi manispaa ya Shinyanga, amedaiwa kunyeshwa sumu na Baba yake mzazi Edsoni Timotheo Damiani (37) kwa kile kilicho elezwa ni kutaka kuficha siri ili mkewe asijui kama amezaa mtoto mwingine nje ya ndoa.

Akielezea tukio leo April 12,2018 Mama mzazi wa mtoto huyo Maria Shija, (22) amesema lilitokea March 24 mwaka huu majira ya saa tatu usiku, ambapo baba wa mtoto huyo alikwenda nyumbani kwao anapoishi yeye na mama yake kwa ajili ya kumsalimia mtoto wake, ndipo akamywesha sumu ya Panya kwa lengo la kumuua.

Amesema wakati kitendo hicho kikifanywa na mzazi mwenzake huyo, alikuwa akimtuma maji ya kunywa mara kwa mara ambapo siyo kawaida yake, na aliporudisha kikombe ndani ndipo akasikia harufu ya dawa ya panya, na aliporudi kwa mtoto haraka akamkuta ameanza kutoa mapovu na mwanaume kukimbia na kopo la Simu ya panya.

“Baada ya kubaini mtoto kapewa sumu nikakimbia kwa jirani ambaye ana fuga Ng’ombe, ndipo nikachukua maziwa nika mnyweshwa, na baadae nikachukua bodaboda hadi kituo cha Polisi kupewa RB na kisha kwenda hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga kupatiwa matibabu, na mtoto wangu ni mzima,”amesema Shija.

”Mwanaume huyu ni Katibu wa CCM Kata ya Kitangili manispaa ya Shinyanga na wakati ananitongoza aliniambia hana mke, na baada ya kuzaa huyu mtoto ndipo akasema ana mke na hamtaki kwani atavunja ndoa yake, na ndio chanzo cha kutaka kumuua kwa kumywesha sumu ya Panya,”ameongeza.

Naye mtu wa Karibu na familia hiyo Jumanne Kagusa, amesema baada ya kuona mtuhumiwa huyo anazangaa mitaani na kutochukuliwa hatua yoyote ya kisheria, ndipo naye akafika kufuatilia suala hilo kwa Jeshi la Polisi, na hatimaye juzi akakamatwa na kuswekwa Rumannde.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi Simon Haule, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na mtuhumiwa yupo mbaroni, na kubainisha kuwa upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.

Maria Shija ambaye ni Mama mzazi wa mtoto aliyenusurika Kifo kwa kunyweshwa Sumu ya Panya na Baba yake mzazi Mume aliyezaa naye, kwa madai ya kuficha Siri kwa Mkewake kuwa amezaa nje ya Ndoa, akielezea namna mkasa mzima ulivyo kuwa hadi kufikia mwanaume huyo kutaka Kumua mtoto waliozaa naye.

Jumanne Kagusa mtu wa Karibu na familia hiyo, anasema baada ya kuona mtuhumiwa huyo anazangaa mitaani na kutochukuliwa hatua yoyote ya kisheria, ndipo naye akafika kufuatilia suala hilo kwa Jeshi la Polisi, na hatimaye juzi akakamatwa na kuswekwa Rumannde.

Majibu ya vipo vya maabara katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga yakionyesha matokeo kuwa mtoto huyo alipewa sumu.

Na Marco Maduhu, ambaye pia ni Mwandishi wa Gazeti la Nipashe mkoani Shinyanga.













Powered by Blogger.