MWANAJESHI MBARONI AKIDAIWA KUGONGA NA KUSABABISHA VIFO VYA WATU WAWILI NA KUJERUHI WAWILI KWA KUWAVUNJA MIGUU


Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga,linamshikilia askari wa jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) Phares Phinehas Chogelo (29) mkazi wa Kata ya OldShinyanga, kwa kosa la kusababisha vifo vya watu wawili na majeruhi wawili, mara baada ya kuwagonga na gari lake lenye namba za usajiri T.105 DGQ Subaru Forest akiwa mwendo kasi.


Akitoa taarifa ya ajali hiyo leo Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simoni Haule, amesema tukio la ajali hiyo limetokea April 8,2018 majira ya saa 5;00 Asubuhi, katika barabara ya Ibinzamata mjini Shinyanga kuelekea Tinde.

Amesema Mwanajeshi huyo akiwa na gari lake hilo aina ya Subaru Forest alimgonga mpanda Baiskeli Steven Joseph (25), ambaye alikuwa amempakiza Nemem Joseph(26) mwanafunzi wa chuo cha uuguzi Kolandoto mjini Shinyanga ,ambapo katika ajali hiyo wote wawili walifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga.

Kamanda amesema pia Mwanjeshi huyo aligonga Pikipiki yenye namba za usajili T .974 BSL aina ya San LG, iliyokuwa ikiendeshwa na Yahya Nasoro (36), akiwa amempakiza Catherine Mwigulu (35), wote wakazi wa mjini Shinyanga, ambapo katika ajali hiyo wamevunjika miguu yote ya kulia.

“Mjeruhi wote hawa wawili ambao wamevunjika miguu bado wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga.”Imesema taarifa ya Kamanda Haule.

Aidha Kamanda alitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mwendokasi, na dereva wa gari hilo ambaye ni Mwanajeshi wanamshikilia kwa mahojiano zaidi na watamfikisha mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili.

Na Marco Maduhu, ambaye ni Mwandishi wa gazeti la Nipashe mkoani Shinyanga.














Powered by Blogger.