RAIS MAGUFULI AAWAPISHA MAJAJI 10 AKIWAMO ALIYEKUWA MKURUGENZI WA KISHAPU- SHINYANGA STEPHEN MAGOIGA





RAIS John Magufuli amewaapisha majaji 10 wa Mahakama Kuu Tanzania, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali , Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, na Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka.


Katika hafla iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam Rais Magufuli amemuapisha Evaristo Longopa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Longopa anachukua nafasi ya Paul Ngwembe ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Edson Makallo ameapishwa kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka, Dk. Julius Mashamba kuwa Wakili Mkuu wa Serikali, na Dk Ally Possi ameapishwa kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.

Siku chache zilizopita Rais Magufuli aliteua majaji wa Mahakama Kuu kwa lengo la kujaza nafasi za majaji waliostaafu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais alimteua Wakili Mkuu wa Serikali na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali kwa lengo la kuhakikisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Mashitaka na Wakili Mkuu wa Serikali zinafanya kazi vizuri kushughulikia masuala ya mahakama.

Majaji wa Mahakama Kuu walioapishwa ni Elvin Mugeta, Elinaza Luvanda, Yose Mlyambina, Immaculata Banzi, na Mustafa Sioyani. Wengine ni Ngwembe, Agnes Mgeyekwa, Stephen Magoiga, Thadeo Mwenempanzi na Butamo Philip.
imeandikwa na Basil Msongo- Habari leo.
Powered by Blogger.