TPA KURASIMISHA BANDARI BUBU
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), inajipanga kurasimisha bandari zote zisizo rasmi (bubu) ili zitambulike rasmi na kuchangia uchumi wa nchi sambamba na kupunguza matukio ya uhalifu.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa bandari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko alisema baadhi ya bandari hizo zimekuwa ni chanzo cha biashara ya dawa za kulevya na biashara za magendo. “Kwa mujibu wa sheria ya sasa ya bandari, moja ya majukumu ya TPA ni kushirikiana na wawekezaji binafsi au wa umma kuweza kuendesha bandari kwa niaba ya serikali... ukishaita bandari hata kama ni ya uvuvi au utalii ni lazima TPA iwepo kwa kuwa yenyewe ndiyo inaangalia ulinzi na usalama kwa niaba ya serikali,” alisema Kakoko.
Aliongeza, “TPA pia ina jukumu la kuangalia suala la afya katika bandari hizo, lakini kwa sasa zipo bandari ambazo hazina maliwato... tunazo ambazo moto ukizuka watu wote watateketea, hivyo ni wajibu wa TPA kuweka uwanja ambao unafuata taratibu na sheria kwa mtu yeyote anayetaka kuendesha bandari mahali popote. Hatutamuondoa mtu yeyote aliyejenga kama wengine wanavyodhani.”
Alisema utaratibu huo pia utawezesha mamlaka zingine ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kukusanya mapato kwa kuwa ni vigumu kwa sasa TRA kwenda mahali ambako bandari haijafafanuliwa au kwenda kwa watu binafsi, hivyo TPA itatengeneza utaratibu utakaorahisisha kukusanya mapato. Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye alisema serikali itaendelea kuiunga mkono TPA na kuhakikisha Bandari ya Dar es Salaam inafanyiwa maboresho makubwa ili kuhakikisha inazihudumia kwa ufanisi, nchi nane zinazoizunguka Tanzania. Alisema katika jitihada hizo za kuboresha bandari, serikali imetenga Dola za Marekani milioni 400 kwa ajili ya kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ikiwemo kufanya upanuzi na kuongeza kina cha maji ili kuwezesha meli kubwa kuingia nchini na kukuza uchumi wa nchi.
imeandikwa na Hellen Mlacky- Habari leo