WAKANDARASI WAPEWA CHANGAMOTO UJENZI BARABARA ZINAZO PITIWA NA MIKONDO YA MAJI


Wananchi wa Kata ya Solwa wakivuka kwenye maji mara baada ya barabara kusombwa na maji na kukatika katikati ,wakilazimika kusomba mpunga kutoka Shambani na kuuvusha kupitia ndani ya maji.


SOMA HABARI KAMILI

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro, amewataka wakandarasi kuwa makini na ujenzi wa barabara ambazo zinapitiwa na mikondo ya maji, ambapo mvua zinapokuwa zikinyesha mfululizo husombwa na maji, na hatimaye kukatisha mawasiliano ambayo hukwamisha kufanyika kwa shughuli za kiuchumi kwa wananchi.

Matiro ametoa rai hiyo leo alipofanya ziara katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga vijijini, ya kutembelea barabara ya Kutoka Kata ya Solwa kwenda Mwakitolyo hadi Kahama, pamoja kwenda Salawe, ambazo zimesombwa na maji na kukatisha mawasiliano.

Amesema wakandarasi wanatakiwa kuwa makini na kutumia ujuzi wao wa hali ya juu katika kujenga barabara ambazo zinapitiwa na mikondo ya maji, kwa kujenga makaravati ya kutosha ili maji hayo yasikose pa kupita, na siyo kuweka machache ambayo husababisha maji kukosa njia na kusomba barabara hizo, kwa kuzi tenganisha katikati.

“Natoa wito kwa wakandarasi barabara hizi ambazo zinapitiwa na mikondo ya maji zinatakiwa ziwe na makaravati ya kutosha, ili kuruhusu maji yapite kwa urahisi, hali ambayo itasaidia barabara kutosombwa na maji,”amesema Matiro.

Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Solwa akiwamo Momo Mathayo, amesema kukatika kwa barabara hizo kumeathiri sana shughuli zao za kiuchumi, ambapo walikuwa wakifanya biashara ya kusafirisha mchele kwenda maeneo hayo lakini hadi ndani ya wiki moja hawafanyi biashara hizo za kiuchumi.

Naye Diwani wa Kata hiyo ya Solwa Awadhi Abood, alisema kukatika kwa barabara hizo mbili kumesababisha hata mapato ya Serikali kushuka, ikiwa biashara hazifanyiki tena, huku baadhi ya wananchi wakilazimika kuvuka kwa kutumia mitumbwi usafiri ambao ni hatari.

Kwa upande wake mhandisi wa Matengenezo kutoka wakala wa barabara mkoa wa Shinyanga (Tanroad) Joseph Mayaya, alisema changamoto iliyopo barabara hizo bado zina maji mengi hasa ya Mwakitolyo, ambapo wanasubili hadi ya Pungue kwanza ndipo waikarabati, huku ya Salawe akiahidi kesho kutwa wananchi wataanza kupita.


Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza mara baada ya kumaliza kufanya ziara ya kukagua barabara hizo za Solwa na Mwakitolyo ambazo zinapitiwa na mikondo ya maji, na hatimaye kusombwa na maji na kukata mawasiliano, na kuwataka wakandarasi wawe wanaweka makaravati ya kutosha kwenye barabara hizo ili kuruhusu maji yapite kwa urahisi.

Barabara ya Kutoka Kata ya Solwa kwenda Kata ya Salawe ikiwa imekatika katikati mara baada ya kusombwa na maji wakati mvua zikiendelea kunyesha na kukata mawasiliano ndani ya wiki moja sasa, huku wananchi wakilazimika kupita ndani ya maji hayo na wengine kutumia mitubwi.

Wananchi wakitoka Kata ya Salawe wakivuka maji kwa kutumia Mtubwi kwenda Kata ya Solwa  mara baada ya barabara kukatika katikati kwa kusombwa na maji.

Wananchi wakiendelea kuvuka maji na kuhatarisha maisha yao mara baada ya barabara ya Solwa kwenda Salawe kukatika.

Vijana wakimvusha mzee.

Mhandisi wa Matengenezo kutoka wakala wa barabara (Tanroad) mkoani Shinyanga Joseph Mayaya (mkono wa kulia ),akitoa maelekezo kwa mkuu wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro kuwa barabara hiyo wataanza matengezo leo ambapo hadi kufikia kesho au keshokutwa wananchi wataanza kupitia kwa muda, na baada ya hapo wataitengeneza vizuri ili kutoathiri shughuli za kiuchumi kwa wananchi.

Barabara ya kutoka Solwa kwenda Mwakitolyo ambayo inapitiwa na Mkondo wa maji ikiwa imekatwa na maji na kukata mawasiliano, ambayo pia hupitika kwenda hadi wilayani Kahama.

Wadau wa maendeleo ikiwamo na Kamati ya Ulinzi na usalama ya wilaya ya Shinyanga wakiangalia barabara hiyo jinsi ilivyokatwa na maji.

Wananchi wakiendelea kupita katika barabara hiyo ya Mwakitolyo ambayo imekatwa na maji mara baada ya mvua kunyesha kwa mfululizo.

Diwani wa Kata ya Solwa halmashauri ya Shinyanga vijijini Awadhi Abood akionyesha mazao yaliyopo mashabani jinsi yalivyo haribiwa na maji.

Baadhi ya mazao yakiwa mashambani yakionekana yalivyoharibiwa na maji wakati mvua zikiendelea kunyesha.

Viongozi wakiendelea kuangalia barabara ya Mwakitolyo jinsi iivyoharibiwa na maji.

Wananchi wakitokea Mwakitolyo kwenda Solwa wakipita kwenye barabara hiyo ambayo imekatwa na maji na kulazimika kutembea kwa miguu, huku magari yao wakiyaacha Ng'ambo ya barabara.

Mhandisi wa Matengenezo kutoka wakala wa barabara (Tanroad) mkoani Shinyanga Joseph Mayaya (mkono wa kushoto ), akimweleza mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro, kuwa barabara hiyo ya Mwakitolyo bado ina maji mengi, hivyo wanasubiri yapungue kwanza ndipo wafanye ukarabati.

Raia wa kichina akitokea Kata ya Mwakitolyo kwenda Solwa akitembea kwa miguu, huku gari yake akiwa ameicha Ng'ambo ya pili, mara baada ya barabara hiyo kusombwa na maji na kumeguka.

Diwani wa Kata ya Solwa Awadhi Abood( mkono wa Kushoto) akibadilishana mawazo na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro.

Na Marco Maduhu ambaye pia ni Mwandishi wa Gazeti la Nipashe mkoani Shinyanga.
Powered by Blogger.