WATU WENYE UALBINO WAFURAHIA KUTOITWA MAJINA MABAYA


Chama cha watu wenye Ualbino Manispaa ya Shinyanga (TAS), wameipongeza jamii kwa kuzingatia elimu kwa vitendo ambayo hutolewa na viongozi wa Serikali na dini, juu ya kuondoa unyanyapaa dhidi yao na kuacha kuwaita majina mabaya ya udhalilishaji.

Hayo yalibainishwa jana na katibu wa chama hicho Lazaro Anael, kwenye kikao cha viongozi wa Kata ya Masekelo manispaa ya Shinyanga, wakati wakifuatilia mrejesho wa mafunzo waliopewa viongozi hao ngazi ya Kata, namna ya kutoa elimu ndani ya jamii ya kuacha kunyanya paa watu hao Albino.

Anael alisema katika mradi wao wa ujumuishwaji watu wenye ualbino ndani ya jamii (ALICN) kwa ufadhili wa Lilian Faundation kutoka Nezeland, ambao unadumu miaka miwili (2017-19) umeonekana kuleta matokeo chanya, ambapo jamii imeacha kuwaita majina mabaya pamoja na kushirikiana nao kwenye shughuli za kiuchumi.

“Mradi huu wa ujumuishwaji watu wenye Ualbino ndani ya jamii tunautekeleza katika Kata 17 za manispaa ya Shinyanga, ambapo mpaka sasa Kata tano zimeshatolewa elimu ya kutonyanyapaa Albino ambazo ni Ndala, Oldshinyanga, Mwamalili, Kolandoto na Ibadakuli, na mrejesho wake unaonekana kuwa mzuri,”Alisema Anael

Naye Zungu Mboje mwenye Ualbino mkazi wa Kata ya Masekelo mjini Shinyanga, alitoa ushuhuda kuwa zamani jamii ilikuwa ikimuita majina mabaya ya udhalilishaji kama vile Zeluzelu, Mbilimelo, lakini kwa sasa majina hayo hayapo tena, na watu ambao humfahamu humuita kwa kutamka majina yake.

Kwa upande wake mtendaji wa Kata ya Masekelo Ester Daudi, alitoa wito kwa jamii kuendelea kuwa na tabia ya kuzingatia elimu mbalimbali kwa vitendo ambazo hutolewa kwao, ikiwamo hiyo ya kutowanyanyapaa watu wenye Ualbino ili wapate kuishi kwa amani na kufanyashughuli zao za kiuchumi.

Katibu wa chama cha watu wenye Ualbino manispaa ya Shinyanga (TAS) Anael Lazaro akizungumza na viongozi wa Kata ya Masekelo manispaa ya Shinyanga juu ya kupanga mikakati ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii ya kutowanyanyapaa watu hao (Albino) pamoja na kushirikiana nao kwenye Shughuli za kiuchumi.

Na Marco Maduhu ambaye pia ni Mwandishi wa Gazeti la Nipashe mkoani Shinyanga.





Powered by Blogger.