WEZI FEDHA ZA TASAF WATAFUTIWA MWAROBAINI


Meneja wa Tathimini wa mfuko wa Tasaf kutoka makao makuu Jijijini Dar es salaam Fariji Mishael wakwanza mkono wa kushoto, katikati ni Mratibu wa Tasaf ambao ndio wa fadhili kutoka benki ya dunia Krishina Pidatala na wa mwisho mkono wa kulia ni Katibu tawala mkoa wa Shinyanga Albert Msovela wakijadilina kwenye kikao cha Tathimini cha mfuko huo wa Tasaf mjini Shinyanga.

SOMA HABARI KAMILI.

Mfuko wa maendeleo ya jamii Tasaf (111) kupitia mpango wa kunusuru Kaya maskini, unatarajia kuanza kulipa fedha walengwa kwa kutumia mfumo wa simu za mkononi, ili zipate kuwafikia wahusika moja kwa moja na kuondoa tatizo la wizi wa fedha hizo.

Imeelezwa kuwa mfumo wa malipo wa sasa wa kwenye makaratasi kulipwa walengwa kupitia waratibu Tasaf wilaya na wajumbe wa Serikali ya kijiji, umekuwa ukikabiliwa na changamoto ya wizi wa fedha hizo na kusababisha baadhi ya walengwa kutopata fedha zao kwa kiwango stahiki.

Hayo yalibainishwa April 20, 2018 na Ofisa wa Teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kutoka Tasaf makao makuu Peter Lwanda, kwenye kikao cha kufanya Tathimini ya ziara yao waliyozunguka ya kukagua maendeleo ya walengwa na kukusanya maoni katika vijiji vitatu vya Isela, Singita na Bukene Shinyanga vijijini.

Alisema mfumo huo wa malipo kwa njia hiyo ya simu kwa walengwa hao wa Tasaf Tayari umeshaanza kufanya majaribio katika halmashauri 16, huku katika maeneo mengine bado wanaendelea na uchunguzi (Research) ili kuona changamoto zilizopo za malipo hayo, na wakishakamilisha mwakani wataanza kuutumia.

“Lengo la malipo ya fedha hizi za Tasaf kupitia mfumo wa Simu za mkononi ni kuwafikia walengwa moja kwa moja, na kuondoa mianya ya wizi wa fedha hizo ikiwamo kuvamiwa njia kwa waratibu pale wanapopeleka fedha kwa walengwa vijijini, pamoja na kupunguza gharama za usafirishaji fedha,”alisema Lwanda.

Naye Mratibu wa mradi huo wa Tasaf kutoka Benki ya Dunia nchini Marekani Krishina Pidatala, alisema katika mfumo huo wa malipo ya fedha za Tasaf kupitia mfumo wa simu za mkononi, amebaini utakuwa na changamoto ambapo wengi wa walengwa hawana simu, mitandao haishiki maeneo yao, na kutokuwa na nishati ya kuchajia simu zao.

Alisema kwa maeneo ambayo yataendelea kukabiliwa na changamoto hizo, hasa za mitandao ya simu kutoshika ikiwamo na ukosefu wa Nishati hiyo ya Umeme ya kuchajia simu zao, bali wataendelea na mfumo huo wa zamani wa kutumia makaratasi, huku akiwataka walengwa hao kujitahidi kununua Simu za mkononi,

Nao baadhi ya walengwa hao akiwamo Gen Maduga, awali wakiwa kwenye mikutano hiyo ya Tathimini walisema kuwa wameshindwa kununua Simu hizo za mkononi kutokana na kiwango cha fedha wanazopewa kuwa ni kidogo, ambazo huzielekeza kwenye madhumuni yaliyokusudiwa na hivyo kushindwa kuweka akiba ya kununua mahitaji mengine.

TAZAMA HABARI PICHA HAPA CHINI


Ofisa wa Teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kutoka Tasaf makao makuu Peter Lwanda, akizungumza kwenye kikao hicho cha Tathimini na kubainisha  mwakani (2019) wataanza kulipa walengwa wote wa Tasaf kupitia simu zao za mkononi ilikuondoa mianya ya wizi wa fedha hizo za Tasaf.

Mratibu wa mradi huo wa Tasaf kutoka Benki ya Dunia nchini Marekani Krishina Pidatala, akizungumza kwenye kikao hicho cha Tathimini, amesema katika mfumo huo wa malipo ya fedha za Tasaf kupitia simu za mkononi, amebaini utakuwa na changamoto, ambapo wengi wa walengwa hawana simu, mitandao haishiki kwenye maeneo yao, na kutokuwa na nishati ya umeme kuchajia simu zao, huku akitoa wito kwa walengwa hao kujitahidi kununua simu ilikufanikisha zoezi hilo.

Meneja wa Tathimini wa mfuko huo wa Tasaf kutoka Makao makuu Jijini Dar es salaam Fariji Mishael, awali akizungumza kwenye kikao hicho cha Tathimini, amesema wamelidhishwa na maendeleo ya walengwa hao ambapo wengi wao maisha yao yamebadilika na kuondoka kwenye ufukara wa kutisha kama hapo awali, huku pia wakiwa wameungwa kwenye mfuko wa bima ya afya CHF.

Joyce Tesha ambaye ni mratibu wa Tasaf kutoka ubarozi wa Sweeden (Programme Officer), naye amepongeza kuona baadhi ya walengwa hao wa Tasaf kutoka Shinyanga vijijini wakiwa na mafanikio, huku wakipeleka watoto wao shule, Clinik, na kutoa wito kwa Serikali ya mkoa wa Shinyanga kutoa elimu kwa walengwa ambao wanafuga mifugo ili kunusuru mifugo yao isife, ambapo baadhi wamekuwa wakikabiliwa na mifugo yao kufa sababu ya kukosa elimu ya ufugaji bora.

Sesil Latemba ambaye ni Ofisa mifumo kutoka Tasaf makao makuu amepongeza kuona watoto wa walengwa hao wanakwenda shule, pamoja na kupata ufaulu mzuri ambapo katika matokeo ya Mwaka jana ya darasa la Saba wanafunzi wote wa walengwa katika shule ya msingi Bukene Shinyanga vijijini, wote walifaulu kwenda kidato cha Kwanza.

Adam Sorensen ambaye ni mratibu wa mifumo ya ulipaji pesa walengwa wa Tasaf kupitia Simu zao za Mkononi, akizungumza kwenye kikao hicho cha Tathimini amepongeza kuona baadhi ya walengwa wa Tasaf Shinyanga vijijini wakiwa na mafaniko, na kusisitiza walengwa wajitahidi kununua simu za mkononi ili kufanukisha zoezi hilo ambalo litasaidia kupata pesa zao kwa wakati na moja kwa moja, ilikuondoa kupitia kwenye mikono ya watu wengi.

Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga DR Rashidi Mfaume, akizungumza kwenye kikao hicho cha Tathimini, amepongeza mfuko wa Tasaf kwa kusajili walengwa wengi kuingia kwenye mfuko wa bima ya afya ya jamii CHF iliyoboresha , ambapo itawasaidia kupata matibabu kwa gharama nafuu.

Mratibu wa Tasaf kutoka halmashauri ya Shinyanga vijijini Happynes Shayo akichangia mada kwenye kikao hicho cha Tathimini, amesema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ufinyu wa fedha ambapo wakati mwingine wamekuwa wakilazimika kukusanya walengwa katika kijiji kimoja ili kuwapatia fedha ,huku wengine wakitoka umbari mrefu na kufanya wengine kushindwa kufika ama kutofika kwa wakati.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga vijijini Bakari Kasinyo, akizungumza kwenye kikao hicho cha Tathimini amesema atasimamie kwa makini zoezi la maofisa maendeleo ya jamii na ugani kutoa elimu ya ujasiriamali kwa walengwa hao wa Tasaf, pamoja na  kilimo cha kisasa, ili wapate kuendelea kuinuka kiuchumi.

Viongozi wa Tasaf kutoka makao makuu jijijni Dar es salaam na ubalozi wa Sweeden, wakiwa kwenye kikao hicho cha Tathimini mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea walengwa wa Tasaf katika vijiji vya Isela, Singita na Bukene Shinyanga vijijini, ilikuona maendeleo yao, pamoja na kukusanya maoni ilikuona changamoto ambazo zinawakabili.

Kikao kikiendelea.

Mratibu wa Tasaf kutoka halmashauri ya wilaya ya Shinyanga vijijini Happynes Shayo (mkono wa kushoto) akiwa na Ofisa mifugo mkoa wa Shinyanga Beda Chamadata.

Kikao kikiendelea.

Katibu tawala mkoa wa Shinyanga Albert Msovela akizungumza kwenye kikao hicho cha Tathimini, baada ya kumaliza kupokea mrejesho na maoni kutoka kwa viongozi hao wa Tasaf, na kuagiza maofisa maendeleo ya jamii na maofisa ugani, kutembelea walengwa wote wa Tasaf na kutoa elimu ya ujasiriamali ambayo itawasaidia kuanzisha miradi ya uzalishaji mali ,na kuendelea kuinuka kiuchumi ikiwa pesa hizo hawatopewa milele, pamoja na kupewa elimu ya kilimo cha kisasa chenye tija.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Shinyanga vijijini Ngassa Mboje (mkono wa kushoto) akiwa kwenye kikao hicho cha Tathimini, pamoja na mhasibu wa halmsahauri hiyo.

Viongozi wa Tasaf kutoka makao makuu,ubarozi wa Sweeden, benki ya dunia na viongozi wa Serikali ya mkoa wa Shinyanga, na halmashauri ya wilaya ya Shinyanga vijijini wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kumaliza kikao cha Tathimini.

Na Marco Maduhu ambaye pia ni mwandishi wa Gazeti la Nipashe mkoani Shinyanga.

















Powered by Blogger.