VIGOGO WALIOTAFUNA FEDHA ZA SHIRECU WAANZA KUZITAPIKA

 Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Takukuru mkoani Shinyanga, imebainisha kuwa vigogo waliokuwa wametafuna mamilioni ya fedha ya Chama cha Ushirika mkoani hapa (SHIRECU), wameanza kujisalimisha mmoja baada ya mwingine na kurudisha fedha hizo.


Imeelezwa baada ya kutolewa agizo la kurudishwa kwa fedha na mali zote za chama hicho na Waziri mkuu Kasimu Majaliwa Januari 13 mwaka huu Jijini Dodoma, mara baada ya watuhumiwa kuitwa waliotafuna na kufilisi mali za vyama vya ushirika, hatimaye wameanza kuzirudisha.
Hayo yamebainishwa leo Mei 4,2018  na Kamanda wa Takukuru mkoani Shinyanga Gasto Mkono wakati akizungumza na vyombo vya habari juu ya utoaji wa taarifa ya utendaji kazi wa Takukuru kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Marchi 2018, kuwa wamepokea taarifa za Rushwa 181, na kufanikiwa kuokoa Shilingi Milion 28,457,000 kutoka katika taasisi mbalimbali.

Alisema moja ya Taasisi hizo ni Chama cha Ushirika Shirecu, ambapo baadhi ya vigogo waliokuwa wametafuna fedha hizo na kukifilisi wameanza kurudisha fedha mmoja baada ya mwingine, ambapo watu hao ni kutoka Katika Kanda mbili za Uzogole na Mhunze Kiasi cha Shilingi Milioni 4,025,000 ikiwa bado kuna Kanda Saba.

Alisema hadi kazi hiyo itakapokamilika ya watuhumiwa hao kurudisha fedha zote, watakuwa wameokoa zaidi ya Shilingi Milioni 200, fedha ambazo zilifanyiwa ubadhilifu kwenye chama hicho cha Shirecu, katika msimu wa kununua pamba mwaka (2012- 2016) ambazo hazikununua zao hilo na kuishia kutafunwa.

“Watuhumiwa hawa wamekuwa wakija mmoja baada ya mwingine kurejesha fedha walizozitafuna, na tunawapatia mwenzi mmoja wawe wameshamaliza marejesho yao, huku wengine tukiendelea kuwafanyia uchunguzi na kuwafuatilia warudishe fedha hizo, na zoezi hili likikamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani,”alisema Mkono.

“Watu ambao wamesalia kurudisha fedha hizo ni kutoka Kanda Saba, ambazo ni za Maswa, Malampaka, Kahama, Meatu, Sola, Lugalu na Bukombe, na tunawaomba wajisalimishe kurudisha fedha hizo za Shirecu kwa hiari yao wenyewe kama wanavyo fanya wengine,”aliongeza.

Pia alitaja taasisi nyingine ambazo walifanikisha kuokoa fedha sababu ya ubadhilifu, kuwa ni Elimu Shilingi Milioni 3,2 ambapo watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga walijilipa malipo ya posho hewa, Ujenzi Milioni 12,2 ambazo zilirejeshwa na Mkandarasi baada ya kubainika alilipwa malipo ya ziada kinyume na mkataba.

Alitaja Taasisi nyingine kuwa ni Madini, ambapo fedha Shilingi Milioni 9.09 zilizokuwa zimekusanywa za mapato ya Serikali kutoka kwa wachimbaji wa wadogo wa madini ya dhahabu, zilikuwa zimefanyiwa ubadhilifu na hatimaye kurejeshwa, na kufanikiwa kwa kipindi chote hicho kuokoa jumla ya Shilingi Milioni 28,547,000.


TAZAMA PICHA HAPA CHINI



Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga, Gasto Mkono akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo kwa kutoa taarifa mbalimbali za masuala ya Rushwa.


Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga, Gasto Mkono akizungumza na waandishi wa habari

Waandishi wa habari mjini Shinyanga wakichukua dondoo muhimu

Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali wakisikiliza taarifa ya Kamanda wa Takukuru mkoani Shinyanga Gasto Mkono.

Kadama Malunde wa kwanza mkono wa Kushoto ambaye ni Mwandishi na Mmiliki wa mtandao wa Malunde 1 blog akiwa na Moshi Ndugulile mwandishi wa Habari Radio Faraja wakisikiliza Taarifa ya Kamanda wa Takukuru mkoani Shinyanga ya kipindi cha Julai 2017 hadi Marchi 2018.

Story na Marco Maduhu ambaye pia mwandishi wa Gazeti la Nipashe mkoani Shinyanga Picha na Kadama Malunde na Mtaalamu Maduhu.

Powered by Blogger.