VILIO VYA TAWALA BUNGENI, BUNGE LA AHIRISHWA
Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson leo asubuhi ameahirisha Bunge mpaka kesho saa tatu asubuhi kupisha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Buyungu Mwl. Kasuku Bilago aliyefariki siku ya Jumamosi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Vilio na simanzi vilitawala katika ukumbi wa Bunge kutokana na kifo hicho cha Mbunge huyo wa Chadema aliyefariki dunia Jumamosi Mei 26.
“Waheshimiwa wabunge, Spika wa Bunge mheshimiwa Job Ndugai anasikitika kuwatangazia kifo cha mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago kilichotokea juzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kwa mujibu wa kanuni zetu, leo shughuli za Bunge hazita endelea na badala yake tutakuwa na maombolezo,” amesema Naibu Spika.
Wakati Naibu Spika Ackson akitoa taarifa za msiba na kuahirisha Bunge, wabunge Julius Kalanga (Monduli), Suzan Kiwanga (Mlimba), Halima Mdee (Kawe) na Dk Semesi Sware (Viti Maalum ) wote wa Chadema walikuwa wakilia.
Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya (Chadema) alishindwa kabisa kujizuia na wabunge walilazimika kumpa usaidizi.
Naibu Spika Dkt. Tulia amesema kuwa Wabunge watakao kwenda kuwakilisha kwenye mazishi hayo wataondoka Dodoma siku ya Jumanne asubuhi na kurejea Dodoma Jumatano mara baada ya mazishi hayo kumalizika.
Pamoja na hayo, Naibu Spika ameendelea kwa kusema "siku ya kesho tutakuwa na kikao cha Bunge kama kawaida isipokuwa tutahairisha Bunge saa sita mchana ili kutoa fursa kwa shughuli za heshima za mwisho kwa mwili wa marehumu Bilago na baada ya hapo tutaendelea na maombelezo hadi siku ya Jumatano"