WATU 30 WAHUKUMIWA KUNYONGWA MAUJI YA ALBINO,VIKONGWE
SOMA HABARI KAMILI
Waziri wa katiba
na sheria Harrison Mwakyembe amesema jumla ya watuhumiwa 30 wa mauji ya
vikongwe na albino hapa nchi wamehukumiwa kunyongwa baada ya kupatikana na hatia
za kuusika na mauji ya watu hao wasio na hatia.
Mwakyembe
amesema serikali itaendelea kutoa adhabu kali kwa watu ambao watabainika
kuendelea kuhusika na mauji ya watu hao ilikuweza kumaliza tatizo hilo ambalo
limeipaka matope nchi ya Tanzania kwa kuonekana sio kisiwa tena cha amani.
Mwakyembe ambaye
pia ni Mbunge wa Kyela aliyabainisha hayo mjini Shinyanga wakati
alipofanya ziara yake ya kikazi, kuwa kwa miaka ya hivi karibuni tatizo la mauji
ya Albino na Vikongwe yamepungua hapa nchini, na watahakikisha wanayakomesha
kwa kutoa adhabu kali kwa wauaji.
“Tatizo hili la
mauji ya vikongwe na Albino linatutia sana doa nchi yetu kimataifa ambayo
imekuwa ikisifika kwa amani na utulivu, hivyo natoa wito kwa wananchi waachane
na mauji ya watu hawa wasio na hatia pamoja na Mahakama zifanye kazi kwa kutoa
hukumu za haraka kwa watu watakao husika na mauji hayo,” alisema Mwakyembe.
Hata hivyo
Mwakyembe alisema serikali itaanza mikakati ya kujenga Mahakama za mwanzo kwa
kila Kata nchi nzima, ilikuondoa misongamano za kesi mahakamani pamoja na
kukarabati majengo ya mahakama ambayo yamechakaa, sanjari na kuwataka wakuu wa
wilaya waunde kamati za maadili za wilaya.
Aidha kwa upande
wake mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack, akisoma taarifa ya mkoa huo alitaja
changamoto ambazo zinawakabili kuwa ni uchakavu wa majengo ya mahakama, uhaba
wa mahakimu pamoja na magereza ya Shinyanga na Kahama kuwa finyu na hivyo
kusababisha mrundikano wa wafungwa.
Na Marco Maduhu.Msukuma Blog