MWANAFUNZI WA CHUO KIKUU ADAIWA KUUAWA KWA KUPIGWA RISASI NA POLISI
Evans Njoroge
Kifo cha Mwanafunzi wa Chuo kikuu nchini Kenya kimezua shutuma mpya za mauaji yanayodaiwa kutekelezwa na maafisa wa polisi nchini humo.
Ripoti zinasema Evans Njoroge, mwanafunzi ambaye alikuwa kiongozi Chuo kikuu cha Meru nchini humo, aliuawa kwa kupigwa risasi na anayedaiwa kuwa polisi.
Mwandishi wa BBC, Ferdinand Omondi anasema picha za mwili wa kijana huyo, damu yake ikionekana imetapakaa kote, zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii huku raia wa Kenya wakighadhabishwa na kile walichodai kuwa mauaji yanayotekelezwa na polisi.
Evans alipigwa risasi Jumanne wakati wa maandamano ya wanafunzi waliokuwa wakilalamikia ongezeko la ada dhidi ya chuo cha Meru.
Vyombo vya habari nchini Kenya vimemnukuu shuhuda mmoja akisema polisi walimkimbiza Evans wakamfikia kisha mmoja wao akampiga risasi na kuondoka.
Mkuu wa polisi Jenerali Joseph Boinnet ameamuru kufanyika uchunguzi kuhusu kifo hicho baada ya kuwepo kwa wanasiasa na makundi ya wanaharakati waliokuwa wakitaka mauaji yanayodaiwa kutekelezwa na polisi kukoma mara moja.