ZITTO AWATAKA WANACHAMA WA ACT WAZALENDO KUJIANDAA KISAIKOLOJIA UCHAGUZI MKUU 2020
Kiongozi wa
chama cha Act wazalendo Taifa Zitto Kabwe, amewataka wanachama wa chama hicho
kujiandaa kisaikolojia katika chaguzi zijazo za viongozi wa Serikali za mitaa (2019)
pamoja na uchaguzi mkuu (2020), kutokana na siasa zinavyoendeshwa hivi sasa kwa
kubinywa kwa uhuru wa demokrasia.
Alisema siasa za
sasa hivi Tanzania ni ngumu, hivyo wasikate tamaa kuendeleza mapambano ya
kupigania demokrasia hapa nchini, pamoja na kuendelea kuulinda mfumo wa vyama
vingi ambao ndio mkombozi kwa watanzania, na waendelee kujipanga kugombea
majimbo katika chaguzi hizo ukiwamo mkuu wa 2020.
Alisema kutokana
na jambo hilo la kubinywa kwa demokrasia hapa nchini, hivyo waanze kujiandaa
kisaikolojia kwenye chaguzi hizo na kutotishika na watu wanaohama vyama vya
siasa, bali waanze kujipanga mapema namna ya kulinda wizi wa kura, kutafuta
mawakala waaminifu, pamoja na viongozi kutatua kero za wananchi.
Zitto
aliyabainisha hayo leo Februari 28 mjini Shinyanga alipokuwa kwenye ziara yake ya kuimarisha Chama alipokutana
kuzungumza na viongozi pamoja na wanachama wa chama hicho mjini humo, kuwa wasiteteleka
na uendeshwaji wa siasa hapa nchini na kuanza kuhama vyama hovyo, bali wajipange
kisaikolojia na kukijenga chama.
“Tunataka chama
chetu kiwe tofauti na vyama vingine vya upinzani kuto hama hama vyama kwa
kuhofia uchaguzi mkuu ujao kuwa hawatopata kura wala uongozi, bali sisi
tujipange kisaikolojia na kufanya kazi ya kusikiliza na kutatua kero za
wananchi, ambao ndio wenye ridhaa ya kutupatia uongozi,”alisema.
Aliongeza kwa
kuwataka viongozi wa chama hicho ambao walipewa ridhaa ya wananchi kwenye
chaguzi zilizopita (2014-15) za madiwani na ubunge wawatumikie wananchi
ipasavyo kwa kutatua kero zao, ili kuonyesha utofauti wa viongozi wa ACT na wa
vyama vingine, ilikuendelea kukiimarisha chama kwa wananchi.
Nao baadhi ya
wanachama hao akiwamo Maarufu Hassani, walionyesha wasiwasi juu ya baadhi ya
viongozi ambao walipata ridhaa kwenye chaguzi zilizopita (2014-15), kuwa kutokana
na vuguvugu la kisiasa hapa nchini la kubinywa kwa demokrasia na chaguzi zinavyoendeshwa,
kuwa kuna uwezekano wa viongozi hao
wasirudi 2020.
Pia katika ziara
hiyo, Zitto alifanikiwa kuvuna wanachama wapya Tisa kutoka vyama mbalimbali vya
siasa, pamoja na kuwapatia kiapo cha utii wa chama hicho, ilikuendelea
kukilinda na kukijenga chama kwa wananchi, ambao ndio watawapatia ridhaa ya
kushika nchi.
TAZAMA HABARI PICHA HAPA CHINI
Katibu wa Jimbo wa chama cha ACT Wazalendo mjini Shinyanga Merkyoli Tafuta, akimkaribisha Kiongozi huyo wa kitaifa Zitto Kabwe, pamoja na kuwatambulisha viongozi mbalimbali wa Chama hicho mkoani Shinyanga na baadhi ya wanachama ambao walihudhulia kikao cha kiongozi huyo ambacho kililenga kuimarisha chama..
Zitto Kabwe ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kigoma mjini ,akiwatoa wasiwasi wanachama wa ACT Wazalendo kuwa nchi hii haiwezi kurudi kwenye mfumo wa chama kimoja licha ya nguvu nyingi kutumika ya kuuwa upinzani, bali kinachopaswa ni kusimama imara na kupigania demokrasia ya kweli, ambayo itawafanya watu kuwa huru na kufanya kile wanachokitaka bila ya kuvunja sheria za nchini, na kuwaasa pia viongozi wa chama hicho waliopewa ridhaa ya kuongoza na wananchi (2014-15) wajitume kufanya kazi ya kutatua kero za wananchi, ili kuonyesha utofauti kati ya viongozi wa ACT na vyama vingine.
Mjumbe wa Kamati kuu ya Chama hicho Taifa Nyangaki Shilungushela, akizungumza kwenye kikao hicho aliwataka wanachama hao wa ACT Wazalendo, kuendelea kujiamini na kufanya kazi licha ya chama chao kubezwa kuwa ni Kichanga na CCM "B" bali wao wasiangalie propaganda za wakosaji ikiwa chama hicho kwa sasa ndio mpinzani wa kweli na ndio kina aminiwa na wananchi katika kuwaletea ukombozi.
Wanachama wa ACT Wazalendo wakiwa kwenye kikao cha kiongozi wao wa chama hicho Taifa ZittoKabwe, na kuaswa kuendelea kukijenga chama na kutoteteleka na siasa za ubinywaji wa demokrasia ambazo zinaendeshwa hapa nchini.
Wanachama wa ACT Wazalendo wakiendelea na kikoa cha kiongozi wao wa kitaifa Zitto Kabwe.
Wanachama wa ACT Wazalendo wakiwa kwenye kikao wakisikiliza ujumbe mbalimbali kutoka kwa kiongozi wao wa chama hicho taifa Zitto Kabwe.
Kikao kikiendelea.
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo mkoa wa Shinyanga Siri Yasini, akimkaribisha kiongozi wa chama hicho Taifa Zuberi Kabwe, kupokea wanachama wapya Tisa ambao wanajiunga na chama kutoka vyama mbalimbali vya siasa.
Kiongozi wa chama hicho Taifa Zitto Kabwe, akimpatia kadi ya chama hicho Mwanachama mpya Ester Mtupili ambaye alikuwa Mwanachama wa Chadema.
Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe akiwaapisha kiapo cha utii wanachama wapya Tisa waliojiunga na chama hicho wakitokea vyama mbalimbali vya kisiasa.
Zitto Kabwe akiwataka wanachama wapya na wazamani kuungana kwa pamoja kukijenga chama, na kuachana na siasa za malumbano, bali wajikite kukipigania chama ilikuendelea kuaminiwa na wananchi ambao ndio wenye ridhaa ya kuwapatia viongozi wengi kwenye chaguzi zijazo ukiwamo uchaguzi mkuu 2020, kwa kuwapatia madiwani wengi ,wenyeviti, na wabunge na hata kushika dola.
Wanachama wa ACT Wazalendo wakipiga picha ya pamoja na kiongozi wao wa chama hicho Taifa Zitto Kabwe.
Na Marco Maduhu, ambaye pia ni Mwandishi wa Gazeti la Nipashe, habari hizi pia utazipata kupitia gazeti la NIPASHE .