WAZIRI WA MAMBO YA NDANI ATOA NENO KWA ASKARI MAGEREZA



Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Dr Mwigulu Nchemba, amewataka askari wa Jeshi la Magereza nchini, kufanya kazi kwa weledi na kufuata kanuni na maadili ya kazi.


Mwigulu aliyasema  hayo  Februari 19 mwaka huu wakati akifungua gereza la wilaya ya chato mkoani Geita .

Alisema  kuna taarifa ya baadhi ya askari magereza wanakeuka maadili ya kazi , pamoja  na kuvunja masharti ya kuhumia wahalifu wawapo magerezani, kwa kushirikiana nao kuwapa simu na vitu vingine, kitendo ambacho ni  kinyume cha sheria na maadili ya kazi yao.

Aliwataka askari hao magereza kila mmoja kuzingatia maadili ya kazi yake, na kuacha kufanya kazi kwa mazoe kama zamani, ambapo hivi sasa majira yamebadilika na wasiwe na urafiki wa kupindukia na waharifu ndani ya gereza.

"Kuna taarifa za rejareja kuwa baadhi ya askari wetu magereza wanawapa simu wafungwa kuwasiliana na jamaa zao, tabia hiyo ilikuwa zamani ambapo walikuwa wanasalimia  familia zao, lakini si sasa ambapo majira yamebadilika unampa simu unadhani anaongea na ndugu zake, kumbe anapanga mipango mibaya,”alisema.

Naye mkuu wa jeshi la magereza nchini kamishna jenerali wa magereza Dk. Juma Malewa, alitaja changamoto kubwa wanazokutana nazo baada ya kufungua gereza jipya,  kuwa ni  uhaba wa usafiri,pamoja na upungufu wa askari, ikiwa gereza jipya linahitaji kuwa na askari wasiopungua 50.

Pia alitaja Changamoto zingine wanazokabilianazo kuwa ni uchakavu wa miundombinu ya magereza, na hivyo kumuomba Waziri huyo awatatulie changamoto hizo ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na weledi.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Geita Gabriel Robert, aliahidi kushirikiana na Jeshi hilo la Magereza, na pia kuwa hakikishia mkoa huo utatoa ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji, ili waweze kupata chakula kingi na kujitegemea katika uchumi hususani pale watakapouza mazao na kupata fedha, na hatimaye kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili.


Powered by Blogger.