MBARAWA AWATAKA MAKANDARASI WAZAWA KUKAMILISHA MIRADI YA UJENZI KWA WAKATI
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na uongozi
wa Wilaya ya Urambo, alipokutana nao katika ziara yake ya kikazi ya kukagua
mradi wa ujenzi wa barabara ya Urambo-Kaliua yenye urefu wa KM 28 inayojengwa
kwa kiwango cha lami, mkoani Tabora.
soma habari kamili
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amewataka makandarasi wazawa wa kampuni ya
Samota, Anam na Jossam JV wanaojenga barabara ya Urambo-Kaliua yenye urefu wa
KM 28 kwa kiwango cha lami wahakikishe wanakamilisha ujenzi wa barabara hiyo
kwa muda uliowekwa.
Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo
katika kijiji cha Motomoto, Wilaya ya Urambo mkoani Tabora alipokuwa katika
ziara yake ya kikazi ya kukagua mtandao wa barabara mkoani humo na
kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo.
“Nataka nione kazi za ujenzi zinafanyika
kwa haraka, kwani uzoefu unaonesha baadhi ya makandarasi wazawa wamekuwa na
kasi ndogo, hivyo mjipange vizuri ili barabara ikamilike kwa wakati”, amesema
Prof. Mbarawa.
Amesema kuwa nia ya Serikali ni
kuwajengea makandarasi wazawa uwezo ili waweze kutekeleza miradi mikubwa
mingine ya ujenzi hapa nchini lakini haitasita kuwanyima kazi hizo kama miradi
hiyo itacheleweshwa, haitakidhi viwango vinavyohitajika na kama hawataonekana
eneo la kazi kwa kipindi kirefu.
“Mkandarasi mzawa atakayechelewesha
mradi wowote wa ujenzi hatapewa kazi nyingine kwa sababu atakuwa amechelewesha
maendeleo ya wananchi”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa Serikali imejipanga
kuwalipa makandarasi wazawa kwa wakati ili waweze kutekeleza miradi yao kwa
ufanisi.
Naye Mbunge wa jimbo la Urambo, Magreth
Sitta, amemueleza Waziri Prof. Mbarawa kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni muhimu kwa
wananchi wa wilaya yake na Kaliua na hata mikoa jirani kwani usafirishaji wa
mazao na abiria utarahisishwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Urambo,
Angelina Kwingwa amesema wamejipanga vyema kutoa ushirikiano kwa wakandarasi
wazawa hao, na kuahidi kumsimamia ili amalize kazi hiyo kwa wakati, lakini kwa
kiwango.
Awali akitoa maelezo ya mradi wa
ujenzi wa barabara hiyo, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani humo Mhandisi
Damian Ndibalinze, amesema mkandarasi ameshapewa fedha za mradi hivyo hakuna
sababu ya kuchelewesha mradi huo na kuahidi kuwasimamia ili wakamilishe kabla
ya mwaka 2020.
Ameongeza kuwa ujenzi wa barabara
hiyo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 37.6 na zote zikiwa zinafadhiliwa na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Tabora-Pangale yenye urefu wa KM 30 inayojegwa na mkandarasi CICO kwa gharama ya shilingi bilioni 28.6 na kumtaka mkandarasi huyo kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ifikapo mwishoni mwa mwezi wa sita.
Waziri Prof. Mbarawa
yuko mkoani Tabora kwa ziara ya siku mbili akiwa na lengo la kukagua
utekelezaji wa miundombinu ya barabara, mkoani humo.
Mbunge wa jimbo la Urambo, Mhe. Magreth Sitta,
akimshukuru Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa
(kushoto), kwa kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Urambo-Kaliua yenye
urefu wa KM 28 inayojengwa kwa kiwago cha lami, mkoani Tabora
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusu hatua za mradi wa ujenzi wa
barabara ya Urambo-Kaliua yenye urefu wa KM 28 na kusisitiza nia ya Serikali ya
kuwajengea uwezo wakandarasi wazawa ili waweze kutekeleza miradi ya ujenzi hapa
nchini.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano