DED Kishapu asisitiza uwajibika kwa walimu

 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga amesisitiza uwajibikaji kwa walimu ili kuleta ufanisi mkubwa katika sekta ya elimu.

Magoiga alitoa msisitizo huo wakati akikabidhi vyumba viwili vya madarasa kwa shule ya sekondari Maganzo wilayani humo vilivyokamilika vyenye thamani ya sh. milioni 19.4.

Vyumba hivyo ni sehemu ya mradi uliotekelezwa na Halmashauri ya wilaya hiyo kutokana na fedha ambazo zilitolewa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Alisema kuwa endapo walimu hao watawajibika ipasavyo wanafunzi watafanya vizuri katika masomo yao na hivyo kuleta sifa nzuri katika shule pamoja na wilaya nzima kwa ujumla.

Mkurugenzi Mtendaji aliongeza kwa kusema kuwa kampeni ya kufuta ziro yaani sifuri inayoendelea itaweza kupata mafanikio makubwa kama walimu watajituma katika kufundisha vizuri.

Aidha aliwataka wanafunzi kujituma na kutumia fursa ya kuwepo shuleni kwa ajili ya kusoma kwa bidii na kufaulu masomo yao hivyo kuweza kuwa watalaamu wa baadaye kwa manufaa ya jamii.

"Itakumbukwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri ilipata ufadhili wa fedha TEA jumla ya sh. milioni 70.5 kati y ash. milioni 141 kwa ajili ya ujenzi wa ujenzi wa miundombinu katika shule hii" amesema.

Alisema kwa kutumia fedha hizo pamoja na kushirikisha nguvu za wananchi inaendelea na ujenzi wa nyumba ya walimu sita.

Kwa upande wake Mkuu wa shule ya sekondari Maganzo, Shija Mbuzimbili alimshukuru mkurugenzi kupitia wafadhili kwa kuwezesha mradi huo ambapo alisema utasaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa.

Alisema umekuwa ni faraja kwa walimu na wanafunzi kwani utasaidia kupunguza mzigo mkubwa kwa walimu kufundisha wanafunzi wengi katika chumba kimoja na wanafunzi wataweza kujifunza kwa nafasi.

Alitolea mfano kuwa hapo awali chumba kimoja kilitumiwa na wanafunzi zaidi ya miaka na hivyo kutokana na mradi huo kukamilika wataweza kuwagawa wanafunzi nusu yake katika vyumba viwili.

Hata hivyo alibainisha bado kuna changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa ambapo aliomba shule hiyo iendelee kupata msaada na kukamilisha kabisa miundombinu mbalimbali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga (mwenye tai) akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Maganzo wakati alipozindua vyumba vya madarasa vilivyokamilika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga akifungua moja ya vyumba vya madarasa vilivyomalika ujenzi wake wakati akivikabidhi kwenye shule ya sekondari Maganzo.

Walimu, wajumbe wa bodi ya shule na wanafunzi (hawapo pichani) wa shule ya sekondari Maganzo wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga (aliyesimama) wakati alipozungumza alipowakabidhi vyumba vya madarasa.
Sehemu ya jengo lenye chumba cha darasa la shule ya sekondari Maganzo lililokamilika ujenzi wake na kukabidhiwa
Powered by Blogger.