WALALAMIKA KUKOSA ELIMU YA UJASIRIAMALI, WASHINDA WAKICHEZA DRAFTI


Picha ni baadhi  vijana wanaoishi Kijiji na Kata ya Bunambiyu wilayani Kishapu wakiwa wanacheza Drafti kijiweni.


Vijana wanaoishi Kijiji na Kata ya Bunambiyu wilayani Kishapu, wameitupia lawama Serikali kwa kushindwa kuwapatia elimu ya ujasiriamali ambayo itawasaidia kupata mikopo asilimia Tano mapato ya fedha za ndani za halmashauri, na kuishia kushinda vijiweni wakicheza drafti.

Wamedai kuwa asilimia kubwa ya vijana ndani ya kijiji hicho wametelekezwa na halmashauri hiyo ya Kishapu, ambapo mikopo asilimia Tano ya vijana wamekuwa wakiisikia vijiji jirani pamoja na vijana hao kupewa mafunzo hayo ya ujasiriamali, lakini wao hakuna kitu kama hicho na kuwafanya kuendelea kuwa tegemezi.

Mmoja wa vijana hao Deogratius Silvester, alisema idadi kubwa ya vijana kijijini humo ni tegemezi kutoka kwa wazazi wao, sababu ya kukosa elimu hiyo ya ujasiriamali ambayo ingewasaidia kupata mikopo na kujikwamua kiuchumi, na kuondokana na dhana ya kushindwa vijiweni wakicheza draft na kuendelea kudumaa kimaendeleo.

“Vijana wa kijiji hiki kama tumetelekezwa na halmashauri hatupati mikopo wala elimu ya ujasiriamali, kila siku tunashinda vijiweni hapa tukicheza draft lakini tungekuwa na elimu hiyo hata kuugwa kwenye vikundi, tungeweza kufanya mambo makubwa pamoja na kuwa na shamba la kikundi tungelima Pamba na kupata fedha.”Alisema Silvester.

Naye Ofisa maendeleo ya jamii kwenye Kata hiyo ya Bunambiyu Neema Nyanda, alikiri kwenye kijiji hicho hakuna vikundi vya vijana waliougwa wala kupewa elimu ya ujasiriamali, na kutolea ufafanuzi kuwa hua ni wabishi sababu wamekuwa wakiitiwa kupewa elimu hiyo hawajitokezi na kukomea wawili au watatu.

Alisema siyo kwamba wamewatenga bali wao wenyewe hawana mutikio wa elimu hiyo ya ujasiriamali, na kukiri ni kweli baadhi ya vijiji jirani vijana wake wanamikopo hiyo asilimia tano ya halmashauri, kikiwamo cha Itongoitale sababu vijana wake waliitikia mafunzo hayo.

Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri hiyo ya Kishapu Steven Magoiga, alisema ili vijana na akina mama wapate kukopesheka asilimia 10 za mapato ya fedha za ndani za halmashauri, lazima wapate mafunzo kwanza ya elimu ya ujasiriamali pamoja na kuungwa kwenye vikundi, tofauti na hapo mikopo hiyo haitolewi.

Alisema fedha mpaka sasa ambazo zimetegwa kwa ajili ya maendeleo ya vijana asilimia Tano ni Shilingi Milioni 93,236,164.86 na kuwasisitiza pale wanapoitwa kwenye mafunzo hayo ya elimu ya ujasiriamali wajitokeze kwa wingi, ili wapate kutumia fursa hiyo kujikwamua kiuchumi na kuondokana na dhana tegemezi pamoja kupunguza tatizo la ajira.

Na Marco Maduhu ambaye pia ni Mwandishi wa Gazeti la Nipashe mkoani Shinyanga.




























Powered by Blogger.