WATU 27 WAUAWA KWA KUKATWA MAPANGA SHINYANGA


Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi (ACP) Simon Haule, amebainisha kuwa jumla ya watu 27 mkoani humo wame uawa kwa kukatwa mapanga, kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo imani za kishirikina .


Kamanda Haule amebainisha hayo leo Marchi 24/2018 wakati akizungumza na vyombo vya habari, kuhusiana na uzushi ambao umekuwa ukienezwa kuwa kwenye Kata ya Salawe tarafa ya Nindo Shinyanga vijijini kuwa kuna watu wanakata mapanga wanawake na kisha kuondoka na sehemu zao nyeti yakiwamo matiti.

Amesema katika mkoa wa Shinyanga hakuna kitu kama hicho, isipokuwa kuna takwimu za wananchi 27 kuuawa kwa kukatwa mapanga kutokana na sababu mbalimbali kwa kipindi cha miaka Mitatu mfululizo kuanzia (2016-18) ambapo Wanawake 12, na Wanaume 15.

Ametaja takwimu hizo kwa kuchambua kila mwaka ambapo mwaka (2016) waliuawa watu 12, Wanawake Sita, Wanaume Sita, (2017) Wanaume Nane, Wanawake Wanne, Mwaka huu (2018) Kuanzia Januari hadi March Wanawake wawili na Mwanaume mmoja jumla watu 27.

Aidha ametaja sababu za mauaji hayo kuwa ni Imani za Kishirikina, Migogoro ya mashamba,kuwania mali, pamoja na wivu wa kimapenzi, na kubainishi kuwa katika matukio hayo Watu 24 wanatuhumiwa kuhusika nayo, ambapo 14 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wakiwamo waganga wa kienyeji na wengine 10 wakiendelea kusakwa.

Pia Kamanda huyo anatoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga kuachana na tabia ya kujichukulia Sheria mkononi bali wafuate sheria za nchi, huku akiwatoa wasiwasi wanawake wa Kata ya Salawe waendelee kufanya shughuli zao za kiuchumi ikiwamo kwenda mashambani, ikiwa hakuna watu watakaotekeleza mauaji.


Na Marco Maduhu ambaye pia ni Mwandishi wa Gazeti la Nipashe mkoani Shinyanga.


Powered by Blogger.