MTOTO WA KIKE AUAWA SHINYANGA KWA KUTENGANISHWA KIWILIWILI, WAUWAJI WAONDOKA NA NYETI ZAKE
Mtoto wa Kike ambaye hajafahamika jina wala makazi yake anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (14-16), ameuawa kwa kucharangwa mapanga na watu wasiojulikana kwa kutenganishwa Kiwiliwili, kwa kukatwa shingo,miguu,kiuno, kuondolewa matiti na sehemu zake za siri, na kisha watu hao kutokomea na viungo hivyo kusikojulikana.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Mei 3, 2018 Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi Simon Haule, alisema tukio hilo limetokea jana majira ya saa 6;00 mchana, katika mtaa wa Jilungi Kata na Tarafa ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga.
Alisema mwili huo wa marehemu ulingulika ukiwa umefungwa kwenye mfuko wa Sandarusi, na kisha kutupwa kandokando ya Barabara kuu ya Shinyanga kwenda Mwanza, eneo ambalo ilibainika kuwa sehemu siyo ya tukio lilipofanyika, bali ni sehemu nyingine ambapo alifanyiwa unyama huo na kutupiwa kwenye barabara hiyo.
“Chanzo cha tukio hili lina husishwa ni Imani za kishirikiana, kutokana na wauaji hao kumkata mapanga mtuhumiwa na kisha kuondoka na baadhi ya viungo vyake vya mwili, na mwili huo umehifadhiwa kwenye chumba cha maiti katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga,” alisema Haule.
Aliongeza kuwa Jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi wa kuwabaini watu waliohusika na mauaji hayo ya kinyama, ili wapate kutiwa nguvuni na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Pia Kamanda alitoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Shinyanga kuachana na vitendo vya kuendekeza Imani za Kishirikina ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu, na kutoa onyo kuwa hatua kali zitaendelea kuchukuliwa dhidi yao.
Na Marco Maduhu ambaye pia ni Mwandishi wa Gazeti la NIPASHE mkoani Shinyanga