ZITTO AMSHUTUMU WAZIRI MAHIGA KUSHIRIKIANA NA ISRAEL
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), ameshutumu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Augustine Mahiga kushirikiana na Israel wakati nchi hiyo inawanyanyasa Wapalestina.
Amesema kwamba uamuzi wa Waziri Mahiga kushirikiana na nchi hiyo haukubaliwi kwa sababu unakwenda kinyume na misingi ya kuwapenda wanyonge iliyoasisiwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere.
“Hivi karibuni Waziri Mahiga alionekana akinywa mvinyo na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wakati Afrika Kusini wamemuondoa Balozi wao nchini Israel baada kutoridhishwa na mauaji dhidi ya Wapalestina yaliyofanywa na Israel.
“Naishauri serikali irudi katika misingi ya kuwapenda wanyonge kwa upendo na amani kama ilivyoasisiwa wakati wa kupandisha Mwenge katika Mlima Kilimanjaro,” amesema Zitto