RC SHINYANGA AHAMASISHA WANANCHI KUTOA TAARIFA SAHIHI UTAFITI WA MAPATO NA MATUMIZI YA KAYA BINAFSI
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Zainab Telack amewataka wananchi mkoani Shinyanga kutoa taarifa sahihi kwa watafiti wanaofanya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi mkoani humo.
Telack ametoa rai hiyo leo Ijumaa Februari 23,2018 katika mkutano na waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga akizungumzia Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/2018.
Utafiti huo unaosimamiwa naOfisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) unaoendelea nchini katika kata 796 utazifikia kaya 9,552 nchini ambapo kaya 408 zitafikiwa katika kata 34 za mkoa wa Shinyanga.
Telack alisema njia pekee ya kufuatilia utekelezaji wa program za maendeleo ni kufanya tafiti mbalimbali kama huu unaoendelea ambao unalenga kutoa takwimu za hali ya umaskini na takwimu nyingine ili kuisaidia serikali na wadau kutathmini hatua zilizofikiwa katika kutimiza malengo ya kitaifa.
“Suala la ukusanyaji wa takwimu rasmi za serikali ni shirikishi na ni wajibu wa kila mwananchi kutoa taarifa sahihi,natoa wito kwa viongozi kuanzia ngazi ya mitaa,vitongoji,vijiji,kata,wilaya na mkoa kutoa ushirikiano wa karibu kwa watafiti watakaozifikia kaya 408 zilichaguliwa katika mkoa wetu”,alisema Telack.
“Utafiti huu wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa mwaka 2017/2018 unahitaji sana ushirikiano kutoka kwa wananchi wote hasa katika kaya zilizochaguliwa kitaalamu kuwakilisha sampuli za kaya zilizopo mkoani Shinyanga”,aliongeza.
Alibainisha kuwa kila kaya iliyobahatika kuchaguliwa itahojiwa kwa siku 14 mfululizo na mdadisi atakutana na mkuu wa kaya ambaye hatatakiwa kubadilishwa ili kupata takwimu sahihi kwa ajili kupanga maendeleo ya nchi.
Mkuu huyo wa mkoa alisema utafiti huo utasaidia kuweka msingi katika kutambua viashiria vya msingi vya kiuchumi,ajira na ustawi wa jamii ambavyo vitatakiwa kufuatiliwa kwa kipindi husika na kupata makadirio ya jumla ya mwenendo wa matumizi ya kaya ili kuandaa fahirisi za bei.
Telack alizitaja kata 34 za mkoa wa Shinyanga zitakazofanyiwa utafiti kuwa ni Ngokolo,Mwawaza,Ndala,Ndembezi,Songwa,Mwadui Lohumbo,Kishapu,Mwakipoya,Lagana,Talaga,Didia,Mwakitolyo,Iselamagazi,Mwamala,Nyida na Lyabusalu.
Kata zingine zitakazofikiwa ni Lyamidati,Lunguya,Chela,Bulige,Jana,Isaka,Chambo,Igunda,Sabasabini,Bulungwa,Ushetu,Ubagwe,Mondo,Nyahanga,Zongomera,Nyihogo,Majengo na Kilago.
Kwa upande wake Meneja wa Takwimu (NBS) wa mkoa wa Shinyanga, Evarist Tairo alisema huo ni utafiti wa saba tangu nchi ipate Uhuru na utasaidia kwa kiasi kikubwa kupata takwimu halisi za mapato na matumizi ya kaya binafsi.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Zainab Telack akizungumzia kuhusu Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/2018 wakati wa mkutano wa waandishi wa habari leo Ijumaa Februari 23,2018 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi yake - Picha na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Zainab Telack akielezea umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi unaoendelea mkoani Shinyanga. Kushoto niMeneja wa Takwimu (NBS) wa mkoa wa Shinyanga, Evarist Tairo. Kulia ni Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Dk. Rashid Mfaume ambaye ni Mganga Mkuu wa mkoa wa Shinyanga.
Waandishi wa habari wakichukua matukio: Telack alisemaUtafiti huo unatarajia kukusanya taarifa kutoka katika kaya binafsi zinazohusu kaya na wanakaya,uzazi na unyonyeshaji,elimu,afya,uraia,uhamiaji,ulemavu,bima,hali ya ajira,biashara na mapato ya kaya na makazi ya kaya.
Waandishi wa habari wakiwa ukumbini: Taarifa zingine zitazokusanywa katika utafiri huo ni matumizi ya nishati,huduma za maji safi na maji taka,utalii wa ndani,uwekezaji wa kaya,matumizi ya kaya ya huduma za kifedha,upatikanaji wa usalama wa chakula,matumizi,kilimo na mifugo pamoja na taarifa za umiliki wa mali kijinsia.
Meneja wa Takwimu (NBS) wa mkoa wa Shinyanga, Evarist Tairo akizungumza wakati wa mkutano huo ambapo aliwasisitiza wananchi mkoani Shinyanga kuwapa ushirikiano wadadisi/watafiti watakazifikia kaya 408 zilizochaguliwa.
Meneja wa Takwimu (NBS) wa mkoa wa Shinyanga, Evarist Tairo akielezea umuhimu wa kufanya tafiti katika nchi.
Waandishi wa habari Sam Bahari (Mtanzania/Rai) na Eunice Kanumba (Kahama Fm) wakifuatilia kwa makini kilichokuwa kinaendelea ukumbini.
Mwandishi wa habari wa habari kutoka Radio Faraja ya Mjini Shinyanga,Moshi Ndugulile akiuliza swali wakati wa mkutano huo.
Mwandishi wa habari wa Channel Ten,John Mponeja akiuliza swali wakati wa mkutano huo.
Afisa Masoko wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Andrew Punjila ambaye pia ni Mhamasishaji wa Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa mwaka 2017/2018 akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo.
Afisa Habari wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Emmanuel Ghulla akizungumza wakati wa mkutano huo.
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Dk. Rashid Mfaume ambaye ni Mganga Mkuu wa mkoa wa Shinyanga akizungumza wakati wa mkutano huo.
Picha ya pamoja Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, waandishi wa habari ,maafisa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Picha ya pamoja Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, waandishi wa habari ,maafisa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
PICHA NA KADAMA MALUNDE NA FRANK MSHANA