ALICHO KIFANYA MAKONDA KWA WANAWAKE 178 WALIOFIKA OFISINI KWAKE
WANAWAKE 178 waliofika kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (pichani) kulalamikia kutelekezwa na baba za watoto wao, wamepatanishwa na wazazi wenzao.
Hayo yalibainishwa jana na Mkuu huyo wa Mkoa, alipokuwa anazungumzia mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kwa kampeni hiyo, Jumatatu iliyopita. Makonda alisema, hatua hiyo ni nzuri kwa kuwa lengo kubwa la mkakati wake ni kusaidia upatikanaji wa haki ya kwanza ya watoto, ambayo ni malezi ikifuatiwa na haki nyingine kama vile upendo na ukaribu.
“Kwa hiyo katika hilo la upendo na ukaribu kwa sasa naweza kusema kuwa limerejea kwa kuwa kama wazazi wote wawili wamekutanishwa na kukubaliana kuendelea na mahusiano yao, hakika mtoto atakuwa mwenye furaha,” alisema Makonda. Alisema tangu kazi hiyo ianze hadi sasa, ofisi yake imewahudumia wanawake zaidi ya 1,498 na ana imani lengo la kuwahudumia wanawake wote waliojitokeza litatimia.
Pia Makonda aliweka wazi kuwa hadi sasa, wapo wanaume ambao wamekubali kupimwa vinasaba (DNA) ili kubaini uhalali wa watoto wanaoambiwa kuwa ni wao. Wakati huo huo, Makonda amezungumzia ujio wa kongamano kubwa la wafanyabiashara wa Ufaransa Jumatatu ijayo.
Alisema,
kampuni 30 za wafanyabiashara kutoka Ufaransa, zitashiriki kwenye kongamano hilo litakalofanyika jijini Dar es Salaam, ambalo kwa kiwango kikubwa litaongeza chachu katika mpango wa serikali wa kufikia uchumi wa kati